
Mwandishi mashuhuri wa habari wa Marekani, amekosoa waziwazi sera za Washington kuhusu Israel, akisema utawala huo ni mzigo mkubwa zaidi wa kigeni kwa Marekani.
Katika mahojiano na mtandao wa Rotana, Tucker Carlson, mwandishi wa habari na mchambuzi maarufu wa Marekani, amekosoa mtazamo wa wanasiasa wa Washington katika kuunga mkono Israel, akiuelezea utawala huo kuwa ni”mzigo mkubwa zaidi wa kigeni” wa Marekani.
Amesisitiza kwamba uhusiano wa karibu kati ya Israel na Marekani kwa sasa unaiathiri Washington na kwamba rasilimali za nchi hiyo zinatumiwa kwa faida ya Tel Aviv.
Akizungumzia juhudi za Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, za kuinyonya Marekani ili kulinda maslahi ya Tel Aviv, Carlson ameongeza kuwa Marekani iko chini ya mashinikizo makubwa ya kutumia rasilimali zake kuanzisha vita vingine huko Asia Magharibi.
Tucker Carlson pia amezungumzia matatizo ya ndani ya Marekani, akisema: “Wakati Marekani inasumbuliwa na changamoto za kiuchumi, umoja wa kitaifa na migogoro ya uhamiaji, viongozi wake wanapaswa kupambana na mashinikizo ya kigeni badala ya kutilia maanani matakwa ya Netanyahu.”
Mwandishi huyo mtajika wa habari wa Marekani amewakosoa vikali maseneta kama Ted Cruz na Lindsey Graham, ambao wanajulikana kwa kuunga mkono utawala wa Israel, akisema kwamba wanasiasa hawa wanatanguliza mbele maslahi ya Israel kuliko maslahi ya watu wa Marekani, na baadhi yao hata wameisaliti nchi yao.