Musoma. Serikali mkoani Mara imeishauri Wizara ya Uchukuzi kuanza mchakato wa ujenzi wa Bandari ya Musoma katika Ziwa Victoria, hatua inayotajwa kuwa chachu ya kufungua fursa za kiuchumi na kuunganisha mkoa huo na masoko ya nchi jirani za Kenya na Uganda.

Ombi hilo limetolewa leo Februari 23, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mtambi, wakati wa ziara ya Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, ambaye yupo mkoani humo kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya wizara hiyo.

Kanali Mtambi amesema ujenzi wa bandari hiyo utakuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi wa mkoa, hasa ukizingatia matarajio ya ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Tanga–Arusha hadi Musoma.

“Usafiri wa majini ni rahisi na utasaidia kupunguza gharama za bidhaa, lakini pia utaunganisha fursa za kiuchumi na biashara kati ya mkoa wetu na nchi za Kenya na Uganda,” amesema Kanali Mtambi.

Amefafanua kuwa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025/50 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025/30, akisisitiza kuwa bandari hiyo itachochea mzunguko wa biashara katika ukanda wa Ziwa Victoria.

Mbali na bandari, Mkuu huyo wa Mkoa pia ameiomba Serikali kuanzisha safari za ndege kutoka Uwanja wa Ndege wa Musoma kuelekea Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam ili kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akieleza jambo kwa Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa alipofanya ziara kwenye mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege Musoma.  Picha na Beldina Nyakeke

Mbunge wa Musoma Mjini, Mgore Miraji, amesema Bandari ya Musoma ilisimama kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 20, hali iliyodhoofisha uchumi wa mji huo.

“Bandari hii ina umuhimu mkubwa kwa uchumi wa Musoma na watu wake. Inapaswa kufufuliwa ili kuunufaisha mkoa wetu,” amesema.

Ameongeza kuwa kutokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika ujenzi wa meli ndani ya Ziwa Victoria, meli hizo zinapaswa pia kufanya safari Musoma na kuunganisha mji huo na miji mingine ikiwamo Kisumu nchini Kenya.

Akijibu hoja hizo, Profesa Mbarawa amesema wizara yake itatuma wataalamu kufanya upembuzi yakinifu ili kuruhusu mchakato wa ujenzi kuanza.

Amesema baada ya kukamilika kwa bandari za Mwanza, Bukoba na Kemondo, sasa ni zamu ya Musoma.

“Serikali imewekeza fedha nyingi katika sekta ya uchukuzi ili kufungua uchumi wa mikoa kupitia usafiri wa anga, majini na barabara. Ujenzi wa Bandari ya Musoma ni jambo la lazima, na tutahakikisha inaanza kutumika ndani ya miaka hii mitano,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Mara, Ezra Daniel, amesema ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Musoma umefikia asilimia 60.

Amesema mradi huo wenye urefu wa kilomita 1.705 unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh36.3 bilioni, na ukikamilika utawezesha kupokea ndege za ukubwa wa kati tofauti na sasa ambapo unapokea ndege ndogo.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wamesema kusimama kwa bandari hiyo kumedorora maendeleo ya mji huo kwa muda mrefu, hivyo wanatarajia kufufuliwa kwake kutaleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi.

“Kufufuliwa kwa bandari hii kutachochea ukuaji wa uchumi ndani ya mji wetu, mkoa na Taifa kwa ujumla. Uchumi wa mtu mmoja mmoja utaimarika sambamba na wa mkoa,” amesema Rajabu Karangi, mkazi wa Musoma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *