Dodoma. Serikali imeitaka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuongeza ushirikiano na sekta binafsi ili kuhakikisha upatikanaji wa takwimu sahihi, zenye uhalisia na zinazokidhi mahitaji ya uchumi wa Taifa.

Agizo hilo limetolewa leo Jumatatu, Februari 23, 2026 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, wakati akizindua Bodi ya tatu ya usimamizi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Bodi hiyo mpya inaongozwa na Spika mstaafu, Anna Makinda, ambaye kabla ya uteuzi wake alikuwa kamisaa wa taasisi hiyo.

Makinda aliteuliwa hivi karibuni na Samia Suluhu Hassan kuongoza bodi hiyo katika kipindi kipya cha uongozi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Luswetula amesema katika dunia ya sasa ya mabadiliko ya haraka ya teknolojia na mifumo ya kidijitali, ushirikiano kati ya taasisi za umma na sekta binafsi ni jambo lisiloepukika.

Amesema sekta binafsi ni mdau muhimu katika ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu kwa kuwa inamiliki sehemu kubwa ya shughuli za kiuchumi, hivyo ushiriki wake utasaidia kupunguza pengo la takwimu na kuongeza ufanisi.

“Tumieni weledi wenu kuzalisha takwimu bora kwa maendeleo ya Taifa. Huduma ya takwimu ni mhimili muhimu katika uchumi, hivyo tufanye kazi kwa kuzingatia maslahi ya wananchi na maendeleo ya nchi,” amesema Luswetula.

Kwa upande wake, Makinda amesema bodi anayoiongoza itaweka mkazo katika uwazi na uwajibikaji ili kuimarisha imani ya umma kwa taasisi hiyo.

Amesema takwimu zisizoaminika haziwezi kuwa na tija kwa watunga sera na wadau wa maendeleo.

“Ni lazima watumishi waaminike na wajenge misingi ya uadilifu. Uwazi utakuwa nguzo kuu ya utendaji wetu, vinginevyo kazi yetu haitakuwa na maana,” amesema Makinda.

Ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko makubwa yanayotokea duniani, ikiwemo matumizi ya teknolojia katika ukusanyaji wa taarifa, watumishi wa NBS wanapaswa kuendelea kujifunza na kujiendeleza kitaaluma ili kukidhi mahitaji mapya ya soko la takwimu.

“Tusichoke kujifunza. Kazi zimeongezeka na zinahitaji utaalamu wa hali ya juu. Ushirikiano wa ndani na nje ya taasisi ni muhimu ili kufanikisha majukumu yetu,” amesema.

Awali, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Amina Msengwa, amesema taasisi hiyo inatambua hitaji la kuwajengea uwezo watumishi wake ili waendane na kasi ya mabadiliko ya teknolojia na mifumo ya kisasa ya uchakataji wa takwimu.

Amesema uongozi umejipanga kutoa mafunzo kwa watumishi wapya na wa zamani ili kuhakikisha wanazalisha takwimu sahihi, kwa wakati na zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

“Wananchi na wadau wa maendeleo wanahitaji takwimu sahihi na kwa wakati. Hili ni jukumu letu. Tutazalisha takwimu zinazoendana na wakati na mahitaji ya Taifa,” amesema Dk Msengwa.

Amebainisha kuwa kwa sasa NBS inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo, ili kuhakikisha takwimu zinazozalishwa zinachochea maamuzi sahihi ya sera, mipango na uwekezaji katika sekta mbalimbali.

Uzinduzi wa bodi hiyo mpya unatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha utendaji wa NBS, hasa katika kipindi hiki ambacho uchumi unazidi kutegemea takwimu sahihi katika kupanga na kupima maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *