SERIKALI imeagizwa iwasilishwe mapendekezo kuhusu namna ya kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi.
Akizungumza na watumishi wa umma wakati akifanya majumuisho ya ziara yake mkoani Kilimanjaro, Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba ametoa agizo kwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kukaa pamoja na kujadiliana ili kupata mapendekezo ya namna bora ya kupunguza gharama za huduma za afya kwa wananchi.
“Kote tulikopita kumekuwa na malalamiko kuhusu gharama katika sekta ya afya. Tengenezeni mapendekezo, kaeni na wenzetu wa TAMISEMI, watumeni makatibu wakuu wakae na kuandaa pendekezo litakalowasilishwa serikalini,” alisema.
Dk. Nchemba amesema kuna familia ambazo kupata Sh 20,000 au Sh 40,000 ni jambo gumu, hivyo endapo kiasi hicho kitatumika kwa ajili ya kumuona daktari pekee, baadhi ya familia hazitaweza kumudu gharama hizo. SOMA: Watu 600 wapata huduma za kibingwa utalii wa matibabu
Amesema kuwa malalamiko ya wananchi yanaonyesha kuwa mgonjwa anapofika hospitalini hulazimika kulipia kufungua faili, kumuona daktari na kufanya vipimo, hali inayosababisha kumaliza fedha zake zote kabla hata ya kupata matibabu kamili.
“Ukiwasikiliza wananchi, utaona kuwa mtu anapofika hospitalini akiwa mgonjwa anaambiwa afungue faili kwa malipo, kumuona daktari alipie, vipimo alipie, na anapogundulika na tatizo tayari fedha zimekwisha. Hali hii haimsaidii sana mwananchi. Hivyo, leteni mapendekezo ili tuishauri serikali namna sahihi ya kushughulikia suala hili,” alisema.
Aidha, amewahakikishia wananchi katika maeneo aliyoyatembelea kuwa serikali itatoa kauli kuhusu kupunguza gharama za matibabu mara baada ya mapendekezo hayo kuwasilishwa na kufanyiwa kazi. “Nafahamu kuwa tupo katika mchakato wa kuhama kutoka utaratibu tuliouzoea kwenda kwenye mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote. Tutaliangalia suala hili na tutatoa kauli baada ya kujipanga vizuri ndani ya serikali,” alisema.
