
Dar es Salaam. Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umekabidhi Sh361.5 milioni kwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) zitakazotumika kukarabati chumba cha upasuaji na kununua vifaa tiba.
Kwa mujibu wa ORCI, wagonjwa 45,000 wa saratani hugunduliwa kila mwaka nchini, kati yao 29,000 wakipoteza maisha.
Akizungumza katika makabidhiano ya hundi hospitalini hapo leo Jumatatu Februari 23, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Diwani Msemo, amesema chumba hicho kitatumika kufanya upasuaji miwili kwa wakati mmoja na kuwa na sehemu za kupumzikia wagonjwa wanne.
“Pia, uchunguzi na huduma hizi zote vitachangia kupunguza vifo vya saratani nchini kwa kipindi cha miaka mitano ijayo,” amesema.
“Pia, kufanya uchunguzi, vyote hivi vitachangia katika kupunguza vifo dhidi ya saratani katika nchi yetu kwa miaka mitano inayokuja,” amesema.
Dk Msemo akielezea umuhimu wa kuwahi matibabu, amesema changamoto iliyopo watu wengi hufika hospitali wakati saratani ikiwa hatua ya tatu na nne.
“Tunamkakati wa kitaasisi na kitaifa katika kupunguza vifo dhidi ya saratani kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2030/31 hivyo tunaboresha huduma zetu. Kitendo cha PSSSF kutuunga mkono ni hatua njema katika kufikia azma hiyo, tunawashukuru sana,” amesema.
Amesema lengo ni kuifanya Ocean Road kuwa kituo jumuishi ambacho kila kitu kitafanyika hapo kuanzia uchunguzi hadi matibabu ikiwamo upasuaji mkubwa katika chumba hicho kipya.
“Wagonjwa wengi watanufaika na hii huduma, kwani kutapunguzwa ucheleweshwaji wa matibabu, kutahakikisha utaratibu mzuri wa huduma, utoaji huduma jumuishi, mwisho tutarejesha matumaini na heshima ya mgonjwa,” amesema.
Mkurugenzi huyo ameomba taasisi na wadau wengine kuunga mkono juhudi hizo huku akisema duniani hakuna Serikali inayoweza kupambana peke yake dhidi ya saratani bila mkono wa washirika.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Fortunatus Magambo, Meneja wa Kitengo cha Uhusiano na Elimu kwa wanachama PSSSF, Omega Ngolle amesema fedha hizo ni sehemu ya mfumo katika kurejesha kwa umma.
“Kati ya fedha hizo, Sh197.1 milioni zitatumika katika ukarabati wa kitengo huku Sh164 milioni zitatumika kununua vifaa tiba na kuvisakinisha (install),” amesema.
Ngolle amesema kwa sasa mfuko wa PSSSF unawanachama zaidi ya 800,000 hivyo wapo watakaonufaika na hatua walioifanya pamoja na wananchi kwa jumla.
Februari 2,2026, Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa alizindua mashine ya PET Scan inayotumika katika uchunguzi wa saratani katika taasisi hiyo ili kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi kwenda nje ya nchi hususan India, ambapo kwa sasa huduma hizo zitakuwa zitatolewa hapa nchini.