
Dar es Salaam. Saa 4:00 asubuhi ya Alhamisi, Februari 19, 2026, katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo, mmoja wa viongozi wa kiroho wa Kanisa Katoliki, alipumua pumzi yake ya mwisho.
Kardinali Pengo alikuwa Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 82. Enzi za uhai wake alijulikana kwa utulivu wake, iwe ndani au nje ya madhabahu, akiwa na sauti ya upole lakini yenye mamlaka.
Hadi anastaafu, alilitumikia Kanisa kama Padre kwa miaka 54, kama Askofu kwa miaka 42 na kama Kardinali-Padre kwa miaka 27.
Ratiba ya mazishi yake itaanza Ijumaa, Februari 27, 2026, kwa mwili wake kupelekwa Kanisa Kuu la St Joseph kwa ajili ya misa itakayofuatiwa na maombi. Jumamosi, Februari 28, 2026, mazishi yatafanyika katika Kituo cha Hija Pugu, Dar es Salaam, mahali alipopachagua kuzikwa enzi za uhai wake.
Mwananchi limefanya mazungumzo na baadhi ya maaskofu waliofanya kazi na Kardinali Pengo, ambao wamesimulia maisha yake, ikiwamo hatua yake ya kuanzisha mwongozo wa fedha katika parokia, kutoka kusimamiwa na Paroko pekee hadi kuhusisha Walei, ili kuweka usimamizi madhubuti.
Maaskofu hao pia wamegusia msimamo wake na namna alivyokuwa akisimamia kile alichokiamini katika masuala mbalimbali. Wamesema alikuwa kiongozi aliyependa umoja wa kitaifa na aliyewapa nafasi ya kutenda waliokuwa chini yake.
Askofu Msaidizi mstaafu, Methodius Kilaini, aliyefanya naye kazi kwa zaidi ya miaka 20 katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, anasema Kardinali Pengo hakuwa mtu wa kuyumbishwa.
“Nimefanya naye kazi miaka 10 nikiwa Baraza la Maaskofu (TEC) kama Katibu Mkuu na miaka mingine 10 nikiwa msaidizi wake. Mara ya mwisho alikuja kwenye Jubilei yangu Machi mwaka jana. Kwa hali yake asingeweza kuja, lakini kwa ukaribu wetu alifika,” anasema Askofu Kilaini.
Anasema katika maisha ya kiroho, misimamo ya Kardinali Pengo ilijengwa katika maadili na mafundisho ya dini. Anamuelezea kuwa alipata shahada ya uzamivu katika maadili kutoka Chuo Kikuu cha Roma.
“Licha ya unyenyekevu wake, alikuwa mwenye msimamo wa maadili na mafundisho ya dini. Hakutaka kuyumbishwa. Alipokuwa anatoa msimamo wake, alizungumza kitu kama kilivyo,” anasema.
Akizungumzia maisha yake ya kila siku, Kilaini, ambaye pia aliwahi kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba kabla ya kuhamia Dar es Salaam, anasema Kardinali Pengo alikuwa mnyenyekevu na mtu wa kawaida aliyezungumza na kila mtu.
“Hata mimi nilipokuwa Baraza la Maaskofu, yeye alikuwa mwenyekiti wangu wa fedha. Sikupata shida yoyote kufanya naye kazi. Kwa kuwa alikuwa Dar es Salaam lilipo Baraza, hivyo yeye ndiye alikuwa jicho la Baraza,” anasema.
Askofu Kilaini anasema jambo jingine lisilosahaulika ni namna alivyosisitiza Walei kuhusishwa katika bajeti za parokia. (Walei ni waumini wote wa Kanisa Katoliki ambao si mapadre, masista au maaskofu).
“Tulifanya kitu kinachoitwa mwongozo wa fedha, maana fedha ndiyo kitu kigumu kukisimamia. Yeye aliweka mwongozo wa Walei kuhusika katika mapato na matumizi. Kabla ya mwongozo huo, Paroko ndiye alikuwa anachukua fedha, anafanya kitu fulani na kutoa ripoti anavyotaka yeye,” anasema.
Parokia 100
Askofu Kilaini anasema jambo jingine litakalokumbukwa ni hatua ya Kardinali Pengo kufungua parokia nyingi.
“Alipoingia kuwa Askofu Mkuu, alitaka kila sehemu iwe na parokia. Kutoka 30 alizozikuta hadi zaidi ya 100 alizoziacha alipoondoka. Habari njema ni kwamba Ruwa’ichi (Yuda Thaddeus, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam) ameendeleza mfumo huo. Kila Kigango kikikaa muda kidogo kinakuwa parokia,” anasema.
Anasema hakuwa mbinafsi na aliwapa nafasi wale aliokuwa akifanya nao kazi, akiwamo yeye mwenyewe. Hakuwahi kupata kigugumizi kufanya naye kazi, kwa kuwa aliwawezesha kuwajibika na hakuwa mtu wa kufanya kila kitu peke yake.
“Alikuwa mlezi. Amewalea viongozi na mapadre wengi. Wengine aliwatuma kwenda kusoma Ulaya na wengine katika vyuo mbalimbali, ikiwamo Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine, ambacho naye alichangia katika uanzishwaji wake.”
“Alikuwa pia mkuu wa kwanza wa Seminari Kuu ya Segerea. Alijua kufundisha vijana na alifurahi kuwa nao. Alipenda watoto, kuna nyakati aliwaalika na kukaa nao kwake Kurasini, maelfu ya watoto,” anasema.
Anasema Kardinali Pengo hakuwa mwongeaji sana bali msikilizaji. Alipokuwa akiwasilisha jambo muhimu, aliongea kwa mamlaka yenye msimamo wa maadili na mafundisho.
Anasema jambo ambalo wengi hawakumuelewa ni mapenzi yake kwa umoja wa Taifa. Kutokana na hilo, kuna nyakati alihusishwa kumpenda mmoja wa viongozi wakuu wa nchi, jambo ambalo halikuwa kweli.
“Yeye hakuwa anataka mgawanyiko. Mara kadhaa aligombana na wengine alipoona kuna dalili za mgawanyiko. Kuna nyakati alisemwa, lakini kwa kuwa hakuwa mwongeaji sana, watu hawakujua anaumizwa kiasi gani. Licha ya maumivu hayo, alibaki kwenye msimamo uleule,” anasema Kilaini.
Kwa upande wake, Askofu Salutaris Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara anamuelezea Kardinali Pengo kama kiongozi aliyesimama kwenye misimamo yake na kusimamia kile alichokisema.
“Nilipokuwa msaidizi wake nilikuta mengi ameshayajenga pamoja na Askofu Kilaini. Japo sikufanya naye kazi kwa miaka mingi kama alivyofanya Kilaini, lakini kwa muda niliofanya naye kazi, alikuwa ni kiongozi aliyesimamia kile alichokisema,” anasema.
Naye Askofu Titus Mdoe wa Jimbo la Mtwara, aliyewahi kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, anamzungumzia Kardinali Pengo kama mtu aliyekuwa akisimamia kile alichokiamini.
“Alikuwa mkimya, hakuwa mzungumzaji sana, lakini alikuwa na misimamo thabiti,” anasema Askofu Mdoe.
Hakutofautiana na waliomtangulia; naye amemtaja Kardinali Pengo kama mtu wa watu, aliyezungumza na kila mtu bila kujali cheo, umri wala wadhifa.
“Alipenda watoto, alikuwa zaidi ya kiongozi,” anasema Askofu Mdoe.