Afrika Kusini. Mwimbaji nyota wa Afrika Kusini, Tyla, ameibua gumzo mitandaoni baada ya kukiri kuwa anavutiwa na staa wa Nigeria, Rema akisema yuko tayari kutoka naye kimapenzi endapo angepata nafasi hiyo.

Mwanadada huyo alikuwa akizungumza katika mahojiano na jukwaa la muziki la kimataifa, Apple Music, ambapo alifafanua mambo mengi kuhusu maisha yake binafsi na safari yake ya muziki.

Ilipofika kwenye maswali kuhusu msanii gani wa kiume anayeweza kutoka naye kimapenzi, alitabasamu na kuweka wazi anampenda Rema na yuko moyoni mwake.

“Nadhani ni mzuri,” alisema Tyla kwa furaha kidogo, kauli iliyosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na kuzua mijadala mikubwa miongoni mwa mashabiki wa muziki barani Afrika.

Mbali na kummwagia sifa, Tyla aliweka wazi kuwa hana tatizo kutoka naye kimapenzi iwapo mazingira yatakuwa rafiki.

“Ningekuwa wazi kwa hilo kama ningepata nafasi,” alisema akionyesha kuwa hana presha wala haraka, bali anaacha mambo yaende kwa mpangilio mzuri.

Kauli hiyo imechukuliwa na mashabiki kama ishara ya ukaribu uliopo kati ya mastaa hao wawili, ambao wote kwa sasa wanatajwa kuwa miongoni mwa vijana wanaotikisa muziki wa Afrika katika soko la dunia.

Mwaka jana kuna picha zilisambaa za wawili hao wakiwa pamoja katika hafla mbalimbali za muziki na kuibua maswali mengi kutoka kwa mashabiki.

Alisema kwa kicheko kuwa baadhi ya picha hizo zilionekana za kimahaba kupita kiasi, wakati kiuhalisia walikuwa wakifurahia tu muda wao kama marafiki na wasanii wenza.

“Watu walifanya zile picha zionekane drama sana kuliko ilivyokuwa kweli,” alieleza.

Tyla na Rema ni sehemu ya kizazi kipya cha wasanii wanaopeperusha bendera ya muziki wa Afrika kimataifa. Wakati Rema akitamba kupitia mtindo wa Afrobeats, Tyla ameifanya Amapiano ipate mashabiki wengi zaidi nje ya mipaka ya Afrika Kusini.

Ukaribu wao, hata kama ni wa kirafiki, unaonekana kuwavutia mashabiki wanaotamani kuona ushirikiano wa kimuziki kati yao. Wapo wanaoamini kuwa kombinesheni yao inaweza kuzaa wimbo mkubwa utakaotikisa chati za kimataifa.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna aliyethibitisha kuwapo kwa uhusiano rasmi wa kimapenzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *