
Viongozi wa kidini nchini Kenya wamelalamika kuhusu hali ya ukame inayokumba kaunti zenye idadi kubwa ya Waislamu huku waumini wakiwa katika mfungo wa Ramadhani.
Baadhi ya kaunti zinazosumbuliwa na ukame nchini Kenya ni Mandera, Turkana, Wajir, Garissa, Marsabit, Isiolo, Kajiado, Kilifi, Kwale, Tana River na maeneo ya Lamu.
Bw. Mohamed Abdulkadir, Mwenyekiti wa Tawi la Baraza Kuu la Waislamu Kenya (Supkem), huko Lamu ameeleza wasiwasi wake kwamba kufunga Swaumu bila maji ya kutosha kunaweza kusababisha upungufu wa maji mwilini, kizunguzungu na kupoteza fahamu, hasa wakati wa joto kali linalohusishwa na ukame.
“Badala ya waumini kuzingatia Swaumu na Swala za pamoja, wanalazimika kuzingatia jinsi ya kuishi kutokana na upungufu wa maji kwa ajili ya wudhu misikitini,” amesema Bw Abdulkadir.
Wakati huo huo, mhubiri wa Kiislamu Mahmoud Ahmed amesema: “Ramadhani ni kipindi ambacho sisi kama Waislamu tunapaswa kufunga. Hakuna kula, wala kunywa maji, kwa angalau saa 14.
“Katika maeneo yaliyoathirika na ukame mkali, kufunga bado inamaanisha kutokula wala kunywa kutoka alfajiri hadi jioni. Kukosa maji safi au hata mahitaji ya kimsingi kunafanya kufunga kuwa hatari, na kuongeza hatari ya kizunguzungu, matatizo ya figo na utapiamlo,” alisema Bw Ahmed.
Mtaalamu wa Lishe katika Hospitali ya Rufaa ya King Fahd ya Lamu, Dkt Rehema Rimba, ameeleza kwamba kufunga wakati wa ukame mkali ni hatari sana.
Kwa mujibu wa Dkt Rehema, joto kali linaongeza upungufu wa maji mwilini na kuathiri usawa wa madini mwilini, jambo linaloweza kusababisha magonjwa.
Amepinga vikali suala la watu wanaosymbuliwa na ukame mkali kufunga Swaumu isipokuwa kama kuna uwezekano wa kusambaza maji katika maeneo yaliyoathirika.
“Kuna haja ya kuwa na mipango ya kuwapa chakula cha msaada. Huu ni wakati ambapo mwili unahitaji maji mengi baada ya kufunga siku nzima, na ikiwa maji hayapatikani, basi afya ya watu inaweza kudorora,” amesema Dkt Rehema.