Kauli na matamshi ya balozi wa Marekani huko Israel, Mike Huckabee, yamesababisha hasira kubwa baada ya kusema kwamba utawala ghasibu wa Israel una haki ya kupanua eneo lake kwa kupora eneo kubwa la Mashariki ya Kati la nchi kadhaa za Kiarabu na Kiislamu, kwa mujibu wa tafsiri maarufu za Torati ndani ya harakati za Kikristo yenye msimamo mkali nchini Marekani.

Matamshi hayo ya balozi wa Marekani huko Israel yaliyotolewa katika mahojiano na mwandishi wa habari wa Marekani, Tucker Carlson Jumatatu iliyopita, yameibua hasira katika duru rasmi za Kiislamu na Kiarabu na kwenye mitandao ya kijamii.

La kuzingatiwa zaidi ni kwamba, mjadala huo haukuishia katika Ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu, bali umeenea hadi ndani ya Marekani yenyewe, huku wanaharakati na wachambuzi wakihoji kama balozi huyo anawakilisha maslahi ya Marekani au maslahi ya Israel?

Wanablogu wa Marekani wanasema Huckabee “hastahili nafasi hiyo” na wametaka nafasi yake ichukuliwe na mtu “asiye wa kundi lake la kidini.” 

Wanaharakati pia wametoa wito balozi huyo arudishwe Washington kwa mashauriano, wakisema kwamba “ni muhimu kwa rais kuonekana akizungumza mwakilishi wake huko Tel Aviv na kurekebisha mwenendo wake.” Wameongeza kuwa “Huckabee anahitaji muda nchini kwake kutafakari kuhusu majukumu yake na mipaka ya uaminifu wake kwa nchi anayoiwakilisha.”

Mwanaharakati mwingine wa Marekani ameandika: “Mike Huckabee anaonekana kuwa balozi aliiye katika nafasi isiyo ya kawaida. Labda ingekuwa sahihi zaidi kumtaja kama mtu anayefanya kazi kwa maslahi ya Israel badala ya maslahi ya nchi yake mwenyewe, ambayo anatakiwa kuifanyia kazi.”

Sauti za Wakristo wa Marekani pia zimejitokeza zikikosoa msimamo wa balozi wa nchi yao huko Israel, Mike Huckabee, huku mmoja wao akiandika: “Lazima tumwombee Balozi Mike Huckabee, ili Mungu amwongoze na kumfungua macho asimame na Wakristo wa Nchi Takatifu, pamoja na kuwa balozi anayewakilisha serikali yetu.”

Mkristo huyo wa Marekani ameongeza kusema: Sikujua kiwango cha uharibifu ambao Israel imewasababishia Wakristo wa ardhi takatifu (Palestina) kwa zaidi ya miaka 70, hadi nilipopata fursa ya kukutana nao na kuwajua kibinafsi huko Yerusalemu, Nazareti na Galilaya.

Itakumbukwa kuwa, mnamo mwaka 2008 Huckabee alifikia hatua hata ya kuhoji utambulisho wa Palestina aliposema, “kiuhakika hakuna kitu cha kipalestina.”

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, imelaani matamshi ya balozi wa US katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel ikisema yanaakisi mawazo ya kikoloni na kuonyesha jinsi Washington inavyoafikiana na miradi ya “udhibti na uunganishaji wa ardhi unaofanywa na utawala wa Kizayuni”.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, pia amesema matamshi ya Huckabee ni “uthibitisho wa wazi wa ushiriki wa moja kwa moja wa Marekani katika vita vya uchokozi vya upanuzi wa utawala wa Israel, pamoja na mauaji ya kikoloni dhidi ya Wapalestina.”

Aidha, ameonya kuwa “kauli zenye  itikadi kali” za balozi huyo wa Marekani zitazidi kuutia moyo utawala unaonyakua ardhi kuendelea na “uhalifu wa kikatili na hatua zisizo halali dhidi ya Wapalestina, sambamba na uchokozi wake wa mara kwa mara dhidi ya mataifa ya eneo hili.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *