
Arusha. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amemwagiza Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Ali Munde kumwelekeza Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuweka mashine ya ukaguzi (scanner) katika Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Namanga (OSBP), ili kurahisisha ukaguzi wa mizigo na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji kodi.
Maagizo hayo yametolewa leo Jumatatu Februari 23, 2026 wakati akizungumza na wananchi wa Mji wa Namanga, wilayani Longido katika ziara yake jijini Arusha.
Dk Mwigulu amesema wanatambua Namanga ni kituo cha biashara na kupongeza mahusiano bora yanayoendelea kati ya Tanzania na Kenya na kutaka waendeleze ujirani mwema wa aina hiyo.
Amesema anatambua kumekuwa na uhitaji wa mashine hiyo mpakani na jambo hilo limeshakuwa la siku nyingi na kumtaka Naibu Waziri huyo amwelekeze Kamishna Mkuu wa TRA ndani ya mwaka huu wa fedha mashine hiyo iwe imeshafikishwa na kufungwa kituoni hapo na ianze kufanya kazi.
“Sisi ngazi ya Serikali kila tunapokaa Rais amekuwa akitutuma kama kuna changamoto tukae tuzitatue wananchi wafanye biashara, shughuli za kiuchumi waweze kujiletea maendeleo.”
“Ninatambua tumekuwa na uhitaji wa scanner hapa mpakani, Naibu Waziri wa Fedha upo jambo hili limeshakuwa la siku nyingi, mwelekeze kamishna jenerali wa mapato ndani ya mwaka wa fedha huu iwe imeshakuja ifungwe ianze kufanya kazi,” amesema.”
“Hili jambo limeshakuwa la muda mrefu muda huo umetosha kufanya manunuzi, imetosha kuweka ‘order’ sasa mashine hiyo ije hapa isaidie wananchi kazi ifanyike kwa kasi,” amesema.
Dk Mwigulu amesema: “Mmekuwa mkiongea sana kuhusu manunuzi nami nilikuwepo huko muda wa kuongeza kasi na mnunuzi umeshatosha ikifika Julai haijaletwa tutahamisha inunuliwe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.”
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amesema kuna uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Kenya na kuna mikutano ya ujirani mwema na wanakwenda mbali zaidi hata michezo na mabonanza kati ya Tanzania na Kenya yatafanyika kupitia wilaya ya Longido.
“Hali ya usalama kwenye mpaka wetu na Kenya ni salama shughuli za biashara mpaka huu ni kubwa siri ya mafanikio ni utulivu, wananchi hawa wanapenda amani na utulivu ambavyo vimewafanya waendelee kufaidika na kukaa katika mpaka huu,” amesema.
Mmoja wa wananchi hao, Habib Mohamed ambaye ni mtaalamu wa mifugo, aliomba vijana warahisishiwe taratibu za mikopo kwa ajili ya mitaji ili waweze kufikia ndoto zao, kwani wanakumbana na changamoto nyingi pindi wanapofuatilia mikopo.
Amesema vijana wa eneo hilo wanaomba mtaji wa ardhi maalumu kutokana na eneo hilo la kifugaji na fursa ya uwepo wa mpaka, hivyo wakipatiwa eneo wataweza kufanya biashara.
“Vijana majirani zetu (Kenya), wametuzidi, wako mbele wana maghala maalumu kwa ajili ya kuhifadhi mazao yao kipindi cha mvua, unakuta kijana umekusanya mahindi hatuna mipangilio maalumu ya kuhifadhi mazao yetu. Wenzetu kule wametengewa na Serikali yao maeneo ya maghala.
“Serikali itusaidie tushindane kibiashara,” amesema.
Katika mkutano huo, Dk Mwigulu alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Longido, kesho kwenda kuchukua tofali zilizowekwa na mvamizi katika eneo siyo lake, baada ya Ofisa Ardhi wilayani humo kuthibitisha kuwa kesi zilizofunguliwa mahakamani mlalamikaji alishinda.
“Kesho tafuta tipa nenda kachukue hayo matofali weka hapo kwa mkuu wa wilaya, haya mambo ya kusumbua watu wanyonge. Kwa hiyo wameangalia wakajua huyu mama atakosa nauli ataacha tu. Mama endelea na ujenzi mkuu wa wilaya shughulikia hilo,”amesema.
Mkazi mwingine ambaye hakujitambulisha amemuomba Waziri Mkuu kuingilia kati wananchi wa mji wa Namanga kulipishwa uniti moja ya maji Sh1,850 kinyume na utaratibu.
Jambo lingine amesema pamoja na kulipa fedha hizo mita hizo zinasoma hewa na wananchi hubambikizwa gharama kubwa za maji.
Pia mwananchi huyo amelalamikia gharama za umeme vijijini kulipishwa Sh302,100 badala ya Sh27,000.
Kuhusu bili ya maji, Waziri wa Maji, Juma Aweso ameielekeza Mamlaka ya Majisafi Arusha (Auswa) kuzingatia bei ya maji wanayotoa mji wa Arusha isilingane na Namanga, kwani maisha ya wananchi wa maeneo hayo hayafanani.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), anayeshughulikia Afya, Dk Jafar Seif akijibu suala la mikopo amesema Serikali haina ubaguzi katika utoaji wa mikopo akielekeza madiwani kushirikiana na maofisa halmashauri katika utoaji wa mikopo hiyo kuwafikia wananchi.