Dar es Salaam. Mwigizaji wa Bongo Movies, Zaiylissa amevunja ukimya na kuwapiga kijembe wale wote wanaomtabiria kwamba ataachika mapema katika ndoa mpya aliyonayo kwa sasa. Wakirejea historia aliyonayo ya kutodumu kwenye ndoa.
Zaiylissa wiki iliyopita alifunga ndoa na mwanaume anayetajwa wa jina la Said, aliyekuwa mchumba wake wa siku nyingi na kuibua maneno mengi mitandaoni. Huku baadhi ya watu wakidai ameolewa mke wa pili na wengine kutoamini kama ni ndoa wakidai ni tangazo.
Hii ni ndoa ya nne kwa Zaiylissa baada ya ndoa zake tatu kuvunjika. Ndoa na mumewe wa kwanza ilivunjika akimtuhumu mwanaume huyo kumpiga, ya pili na msanii wa muziki wa singeli, Dullah Makabila, ilidumu kwa miezi mitatu tu, kabla ya kuolewa na Ofisa Habari wa zamani wa klabu za Simba na Yanga, Haji Manara.
Ndoa iliyopata umaarufu mkubwa, hata hivyo haikudumu kwa muda mrefu kabla ya kuvunjika, hali iliyozua mjadala mpana kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. Manara na Zaiylissa walifunga ndoa Januari 24, 2024 lakini kufikia Aprili 12, 2025 ndoa hiyo ilikuwa imeshavunjika.
Akizungumza na Mwananchi, Zaiylissa amesema ndoa yake mpya na Said sio maigizo na kuitaka jamii iache tabia ya kuhukumu vitu bila kujua ukweli wa mambo, akisema yaliyotokea ndani ya ndoa zake zilizopita anayajua yeye.
“Watu wengi wanaongea bila kujua ukweli, kuachika sio dhambi, na sio kila ndoa inalazimika kudumu, kikubwa ni amani ya moyo na heshima, hivyo kwa ndoa hii sifikirii kuachika, nimeelewa kweli,” amesema Zaylissa.
Aidha, Zay amesema haoni sababu ya kujitia unyonge katika ndoa yake hii kwa sababu tu ndoa zake zilizopita hazikudumu, akisisitiza daima aliamini ipo siku atapata ndoa yenye mafanikio.
“Mimi naamini ndoa ni jambo la kheri na sitaacha kuolewa kwa sababu ya hofu ya kuachika, maisha ni safari na kila hatua inanifundisha kuwa imara zaidi. Nilikuwa naomba Mungu nipate mwanaume ambaye naweza kudumu naye ndiyo huyo sasa Side wangu,” amesema.
Kuhusu habari ya kuolewa mke wa pili, jambo ambalo limezua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na wadau wa burudani nchini, Zaylissa amesema:
“Mimi siyajui hayo na kama iko hivyo, sioni tatizo katika uamuzi wangu kwani nimechagua kufanya kile kitu kinachonipa furaha.Sio kila ndoa inafanana na sio kila mwanaume anafanana, nilichojifunza ni kutanguliza amani yangu, kama nimeamua kuolewa ni kwa sababu nimeona thamani yangu katika maisha yangu,” amesema.
Nyota huyo wa tamthilia ya Jua Kali, amesema maneno ya watu hayabadilishi mwelekeo wa maisha yake, hata akiolewa mke wa pili au wa tatu, ndio ameshaolewa.
“Watu wanaweza kusema chochote, lakini hawaishi maisha yangu, mimi najua maumivu niliyopitia na najua sababu ya uamuzi wangu. Sitaki kuishi maisha ya kuigiza ili kufurahisha watu na pia kama nimeolewa mke wa pili au wa tatu nazo ni ndoa na ndio nishaolewa sasa,” amesema.
Zaylissa pia aliwataka watu kuacha kuhukumu wanawake wanaoanza upya baada ya kuachika, akisema kila mtu ana haki ya furaha.
“Hakuna anayepaswa kuogopa kuanza upya, kuachika sio mwisho wa maisha, kama kuna nafasi ya furaha, mwanamke ataendelea kuolewa bila hofu,” amesema.