
Afrika Kusini inajiandaa kufuta zaidi ya viza 2,000 ambazo zimepatikana kwa njia isiyo sahihi, huku serikali ikiendesha msako mkali wa kupambana na rushwa ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Waziri wa Mambo ya Ndani Leon Schreiber amesema, mamlaka zinapitia mchakato wa kiuendeshaji kubatilisha viza ambazo zinaaminika zilitolewa kupitia mitandao ya rushwa baada ya mfumo wa uhamiaji kuchezewa.
“Tunaangalia mchakato wa kiuendeshaji ili tufute zaidi ya viza 2,000 ambazo zimetolewa kwa njia ambayo sio sahihi,” amesema Schreiber.
Hatua hiyo inafuatia uchunguzi wa kina uliofanywa na Kitengo Maalumu cha Uchunguzi (SIU), ambacho kimeibua nyaraka zilizoghushiwa, utoaji na upitishaji wa viza usio wa kawaida, na mtandao wa uwezeshaji unaoruhusu watu kuingia Afrika Kusini kinyume cha sheria.
Schreiber amewaambia waandishi wa habari mjini Pretoria kwamba hatua za kinidhamu tayari zimechukuliwa dhidi ya maafisa waliopatikana na hatia.
Tangu Aprili mwaka jana, maafisa 20 wa Mambo ya Ndani wamefutwa kazi na wengine 16 kusimamishwa kwa muda.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa serikali, mfumo wa Afrika Kusini wa uhamiaji umetumiwa vibaya kwa miaka mingi na kundi dogo la maafisa ambao wamejitajirisha, kwa kupokea malipo mkabala wa kutoa viza, na vibali vya kuishi…/