Madrid, Hispania. Licha ya kupewa kifungo cha awali cha mechi moja kwa tuhuma za ubaguzi wa rangi, mshambuliaji Gianluca Prestianni ni miongoni mwa nyota ambao wamesafiri na Benfica leo Jumanne, Februari 24, 2026, kwenda Hispania kwa ajili ya mechi ya marudiano ya hatua ya mchujo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid kesho Jumatano.
Prestianni anatuhumiwa kumbagua kwa rangi nyota wa Real Madrid, Vinicius JR katika mchezo wa kwanza baina ya timu zao uliochezwa wiki iliyopita katika Uwanja wa Da Luz, Lisbon Ureno ambao ulimalizika kwa Real Madrid kupata ushindi wa bao 1-0.
Wakati Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (UEFA) ukiamua kumsimamisha Prestianni kwa mechi moja huku ikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo la ubaguzi analohusishwa nalo, Benfica imeamua kwenda naye Hispania ikionekana inaendelea kumuunga mkono mchezaji huyo kwenye sakata lake.
Winga wa Real Madrid, Vinicius Jr (akiwa kushoto) katika mgogoro na nyota wa Benfica, Gianluca Prestianni wakati akidai kutolewa maneno ya kibaguzi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa Februari 17, 2026. Picha na Mtandao
Benfica inaendelea kuamini kuwa uamuzi wa kumsimamisha Prestianni sio sahihi na umekata rufaa kuupinga ikiamini kwamba uamuzi wa UEFA utabatilishwa na kesho mchezaji huyo atacheza dhidi ya Real Madrid
Rais wa Benfica, Rui Costa ameonekana kushangazwa na uamuzi wa kumsimamisha Prestianni ili kufanya uchunguzi akiuita sio wa haki.
“Hakuna kilichothibitishwa na kukosekana kwa mchezaji katika mechi hii hakuhalalishwi. Prestianni anaitwa mbaguzi wa rangi lakini yeye sio mbaguzi wa rangi hata kidogo. Naweza kuthibitisha hilo,” amesema Rui Costa.
Winga wa Real Madrid, Vinicius Jr akiwa katika mgogoro na nyota wa Benfica, Gianluca Prestianni wakati akidai kutolewa maneno ya kibaguzi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa Februari 17, 2026. Picha na Mtandao
Kama Prestianni atabainika kuwa na hatia ya ubaguzi wa rangi, atafungiwa hadi idadi ya michezo 10.
Staa wa Real Madrid, Kylian Mbappe ni miongoni mwa waliomuunga mkono Vinicius Jr wakati nyota hiyo wa Brazil aliporipoti tukio hilo kwa Refa Francois Letexier mara baada ya kutokea. Hata hivyo, Prestianni amedai kuwa Mbappe alitafsiri vibaya kile ambacho amekisikia.