Nigeria. Supastaa wa Nigeria, Davido ametangaza kujiondoa katika kesi ya malezi inayomkabili Sophia Momodu, mama wa binti yake Imade Adeleke.
Msanii huyo wa Afrobeats, alisema hakuwahi kuomba malezi ya mtoto, bali alitaka wamlee mtoto wao pamoja kama wazazi ili kuepusha migongano ya kifamilia.
Kupitia machapisho kadhaa kwenye akaunti zake rasmi za X na Instagram, Davido alisema hakuna cha kusherehekea katika mzozo huo wa kisheria na kwamba uamuzi wake wa kuondoa kesi mahakamani ni kwa ajili ya mtoto wake.
“Sikuomba malezi kamili niliomba malezi ya pamoja hakuna aliyeshinda, hakuna aliyepoteza isipokuwa Imade sijui kwa nini baadhi ya watu wanasherehekea jambo hili,” aliandika Davido.
Davido alimkosoa wakili Ebelechukwu Egeonu aliyekuwa anasimamia kesi hiyo, akimtuhumu kufanya mchakato wa kesi kuwa mgumu zaidi lakini wakili huyo hajatoa tamko lolote hadharani.
Kesi hiyo inaendelea katika Mahakama Kuu ya Jimbo la Lagos. Shauri hilo lilifunguliwa Aprili 17, 2024, likiwa na lengo la kumruhusu Davido kupata haki ya kumuona na kumlea Imade bila vikwazo.
Katika kikao cha Julai 5, 2024, mbele ya Mahakama ya Familia ya Yaba, Lagos, pande zote zilihudhuria. Timu ya mawakili wa Davido, ikiwemo Dk. Olaniyi Arije na Okey Barrah, ilidai kuwa msanii huyo ametimiza wajibu wake wa kama baba kwa kulipa ada za shule, kugharamia usafiri na makazi ya Imade.
Kwa upande wake, Sophia Momodu alidai kuwa Davido alimtelekeza mtoto wao kwa kipindi cha miaka miwili na kusitisha majukumu yake ya kifedha, hivyo kumlazimu yeye kugharamia kodi ya nyumba, matumizi ya kila siku, safari, matibabu na mahitaji mengine ya mtoto.
Timu ya mawakili wa Sophia pia ilieleza kuwa mtindo wa maisha wa Davido unaojumuisha safari za mara kwa mara, mijadala ya hadharani na kuhusika na watu wengi katika mzunguko wake haukufaa kwa malezi ya mtoto. Walitaja pia ndoa yake mpya na kifo cha mwanawe kama sababu zinazofanya Imade asiwekwe chini ya malezi yake pekee.
Imade Adeleke, binti wa kwanza wa Davido, alizaliwa mwaka 2015 na mara kwa mara ameonekana kwenye machapisho ya wazazi wake mitandaoni. Hadi sasa, hakuna tangazo rasmi la mahakama lililotolewa kuthibitisha rasmi kuondolewa kwa kesi hiyo.