
Dar er Salaam. Sweta la cashmere, ukubwa wa XXL, zawadi kwa mwanafalsafa mwenye heshima kubwa Marekani, Noam Chomsky. Mkoba wa Goyard purse kwa ajili mtangazaji maarufu Marekani, Peggy Siegal.
Saa ya Rolex kwenda kwa mtu ambaye jina lake limefichwa. Hayo ni mambo ndani ya Mafaili ya Epstein, yaliyoachiwa na Wizara ya Habari Marekani (DOJ).
Zawadi ya begi la mkononi la Prada kwa ajili ya mwekezaji wa Kirusi, Masha Drokova. Nyaraka zimeonesha kuwa Epstein alitoa Dola 1,790 za Marekani (Sh4.654 milioni) kulipia zawadi hiyo. Barua pepe za Mafaili ya Epstein, zimeonesha alinunua nguo za ndani (boxer) 31 za Sea Island, mashati ya pamba 31 ya Sea Island, ukubwa wa kati (medium), chata ghali ya Zimmerli. Hizo zilikuwa kwa ajili ya veterani wa filamu Hollywood, Woody Allen.
Nguo hizo za ndani na mashati kwa ajili ya Woody Allen, Epstein alilipia Dola 9,858 za Marekani (Sh25.63 milioni). Watu wengi waliopewa zawadi na Epstein, DOJ imehariri majina yao ili wasionekane. Presha ya umma ni kuwa kila kitu kiwe wazi ili hatua zinazostahili zichukuliwe, kwa kila atakayebainika alitenda uhalifu kwa kushirikiana na Epstein.
Mwanamitindo wa Ukraine, Anastasia Nochnaya (Nastia N), ametajwa kuwa mmoja wa waliokuwa wakimtafutia wasichana Epstein.
Kwa kazi hiyo, Epstein alimzawadia tiketi ya ndege, akafadhili masomo yake Marekani, akamnunulia na kompyuta mpakato, MacBook ya Dola 3,500 za Marekani (Sh9.1 milioni).
Mhalifu huyo wa ngono kwa mabinti wadogo, alipokuwa anataka kujiweka karibu na wanazuoni ili kujijengea imani na uhalali kijamii, alihakikisha anasaidia programu za vyuo kifedha. Chuo Kikuu cha Harvard ni mfano unaojitosheleza. Nyaraka kutoka kwenye Mafaili ya Epstein na Jarida la Harvard, vinathibitisha.
Jarida la Harvard liliandika kuwa, Epstein alitoa michango yake kwa chuo zaidi ya mara 40, kati ya mwaka 2010 na 2018. Jarida limeandika kuwa Epstein alitembelea pia mara kwa mara Kituo cha Utafiti wa Mchakato wa Mabadiliko, Kibaiolojia na Sayansi ya Jamii (EPD). Nyaraka moja inaonesha alichangia Dola 6.5 milioni za Marekani (Sh16.9 bilioni).
Katika chuo hichohicho, Harvard, Epstein alichangia kwenye taasisi ya sanaa, Hasty Pudding Institute of 1770, Dola 50,000 za Marekani (Sh130 milioni), kila mwaka. Hata hivyo, kuna miaka Epstein alichangia zaidi ya kiasi hicho. Mathalan, kuna nyaraka zimeonesha alichangia Dola 225,000 za Marekani (Sh585 milioni). Mwaka 2013, inaonesha alichangia Dola 75,000 za Marekani (Sh195 milioni).
Rais wa Harvard, Lawrence Bacow, katika taarifa yake ya majuto kuhusu taasisi yake kujifungamanisha na Epstein, alisema kuwa walipokea Dola 9 milioni za Marekani (Sh23.4 bilioni), kutoka kwa Epstein, kabla ya mwaka 2008.
Akasema, baada ya Epstein kutiwa hatiani kwa makosa ya usafirishaji wa mabinti wadogo kwa ajili ya ngono na ukatili wa kingono kwa wasichana, wao kama chuo walijitenga naye na hawakupokea zawadi yoyote kutoka kwake.
Bacow, aliyeshika uongozi wa chuo Juni 2025, alisema jumuiya zote za Harvard zinachukizwa na uhalifu wa Epstein, na kwamba chuo hicho kinatambua kuwa kupokea fedha za mhalifu huyo ilikuwa fedheha hata kwa wafadhili.
Pamoja na utetezi huo, shida ipo kwenye nyaraka za kwenye Mafaili ya Epstein, ambazo zimeonesha kuwa, Harvard waliendelea kupokea fedha za Epstein, hata baada ya kutiwa hatiani na kufungwa jela.
Kanuni ya Epstein kutoa zawadi kupata alichopata, haiishii tu Harvard, bali vyuo vikuu mbalimbali Marekani, ikiwamo Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT), iliyopokea Dola 850,000 za Marekani (Sh2.21 bilioni), kati ya mwaka 2002 na 2007.
Chuo Kikuu cha Yale, Columbia, California, na Los Angeles, ni baadhi ya vyuo vikuu vilivyonufaika na mgawo wa fedha kutoka kwa Epstein.
Ufadhili huo wa Epstein na mpango wa mhalifu huyo wa ngono kwa watoto wadogo kuwaweka karibu wanazuoni, vimesababisha zahama kwa taasisi za kubwa za elimu Marekani.
Vyuo vikuu vya Yale, Columbia, California, na Los Angeles, vimelazimika kuwaweka kando baadhi ya maprofesa wake, ambao wameguswa na Mafaili ya Epstein na ambao waliziunganisha taasisi hizo na mpango wa kifedha kutoka kwa mhalifu huyo.
Chuo Kikuu cha Arizona, kimeahirisha Kongamano la Kisayansi, lililokuwa lifanyike Aprili 2026, baada wazungumzaji wengi waliokuwa wamepangwa pamoja na baadhi ya waratibu, kutajwa kwenye Mafaili ya Epstein.
Mfano, mmoja wa waratibu, mwanabaiojoloji Stuart Hameroff, Februari 6, 2026, aliandika kwenye mtandao wa X, akikiri kuwahi kupokea fedha kutoka kwa Epstein, kwa ajili ya Komangamano la Kisayansi.
Rais wa Chuo Kikuu cha Bard, Leon Botstein, ni miongoni mwa viongozi wa wanazuoni na watafiti, ambao wamekiri kuwa walikutana na Epstein kwa lengo la ukusanyaji fedha.
Alichokisema Botstein ndicho kinachosafiri chuo hadi chuo, na kwa sababu Epstein alijiweka wazi kama mtu mwenye kujitoa kwa ajili ya maendeleo ya kitaaluma, maprofesa wengi waliuingia mtego.
Gazeti la New York Times, liliripoti kuwa ilikuwa nadra kwa Epstein kutimiza ahadi zake za kuchangia vyuo. Hata hivyo, nyaraka za Mafaili ya Epstein, zilizowekwa kwa umma Januari 30, 2026 na Wizara ya Haki Marekani (DOJ), zimeonesha mamilioni ya dola, ambayo Epstein aliweza kuchangia kwenye shughuli mbalimbali za vyuo, hasa utafiti na makongamano.
Fedha za Epstein zimesababisha mjadala mzito katika jumuia ya wasomi, hasa Marekani.
Vyuo vyote vimekuwa na mzigo mzito wa utafutaji fedha kwa ajili ya kuhudumia vitivo, utafiti na makongamano. Taarifa za ufadhili wa Epstein vyuoni zimeibua maswali ya jinsi utafutaji huo wa fedha unavyozingatia maadili, je, watu wanaochangia ni safi na pesa zao ni halali?
Mjadala huo unatokana na taswira iliyopo kwa umma hivi sasa kwamba fedha za Epstein zimeinajisi elimu Marekani.
Epstein siyo tu alikuwa mhalifu wa ngono kwa mabinti wadogo, bali pia fedha zake zilikuwa chafu. Aliwaingiza mkenge matajiri na kujipatia fedha isivyo halali. Wengi aliwaingiza kwenye uhalifu wa kingono na mabinti, kisha aliwarekodi. Ushahidi huo aliutumia kuwafanya matajiri kuishi kama mateka wake, hivyo kujipatia utajiri mkubwa kutoka kwao.
Mabilionea, Leslie Wexner na Leon Black, tayari walishakiri hadharani kuwa walitapeliwa na Epstein. Sehemu ya ujumbe ulioachwa wazi kutoka kwenye Mafaili ya Epstein, umeonesha jinsi Epstein alivyokuwa anamtisha Black ili ampe fedha. Ikaonesha namna alivyokuwa anawasaidia matajiri kucheza na namba ili kuikosesha Serikali mapato, kisha yeye kujitengenezea kamisheni ya mamilioni ya dola.
Sasa, mtu wa aina hiyo, na njia zake zote chafu, ikiwamo kuwatumia mabinti wadogo kama silaha yake kuwanasa matajiri ili wampe utajiri. Kuwaandaa mabinti kutoa huduma ya ngono kwa matajiri na kuwarekodi.
Kuwapitisha wasichana kwenye mateso makali ili kuwasterehesha wateja wake. Mtu huyo anapokuwa mfadhili wa elimu, hapo ndipo palipo na maswali kuhusu ulinzi wa hadhi ya elimu, na utakatifu wake.
Itaendelea kesho.