
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Fuad Hussein amesema, uundaji wa serikali mpya ya nchi hiyo ni “suala la ndani,” ukiwa ni mjibizo uliotolewa wiki chache baada ya Marekani kutishia kufuta msaada na uungaji mkono wake kwa nchi hiyo ya Asia Magharibi.
Taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Iraq imesema: akizungumza mjini Baghdad katika mkutano na Tom Barrack, balozi wa Marekani nchini Uturuki ambaye pia ni mjumbe maalumu wa Washington katika masuala ya Syria na Iraq, Hussein amesisitizia “umuhimu wa kudumisha mawasiliano na uratibu katika awamu ijayo hadi mchakato wa kuunda serikali ya Iraq utakapokamilika”.
Mwezi uliopita, muungano mkuu wa kisiasa wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq, ambao una wingi wa wabunge, ulitangaza kumteua waziri mkuu wa zamani Nouri al-Maliki kuwa mgombea wake wa nafasi ya uwaziri mkuu.
Mapema mwezi huu, mshauri wa serikali ya Iraq alifichua kwamba Washington ilikuwa imetuma ujumbe kwa muungano wa Mfumo wa Uratibu, ikionya kuhusu vikwazo vinavyowezekana kuwekwa na Marekani iwapo kambi hiyo itaendeleza msimamo wa kumfanya al-Maliki mgombea wa uwaziri mkuu.
Mshauri huyo ambaye hakutajwa jina alisema mnamo Februari 16 kwamba Marekani imetishia kuweka vikwazo dhidi ya Shirika la Masoko ya Mafuta la Serikali (SOMO), Benki Kuu ya Iraq, sekta za usalama na kidiplomasia, pamoja na wanasiasa na maafisa wa zamani na wa sasa, hatua ambazo imeelezwa kwamba zinaweza kukaribia kusimamisha biashara ya kimataifa ya Iraq na kutoa changamoto hata kwa ulipaji mishahara ya sekta ya umma.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Al-Maliki mwenyewe ameeleza katika mahojiano na AFP siku ya Jumatatu kwamba hatajiondoa katika kugombea licha ya vitisho vya Rais wa Marekani Donald Trump vya kukomesha uungaji mkono na misaada yote ya Washington kwa Iraq ikiwa yeye atachukua wadhifa wa waziri mkuu.
“Sina nia kabisa ya kujiondoa kwa heshima ya nchi yangu, uhuru wake, na utashi wake. Hakuna mtu mwenye haki ya kusema ni nani tunaweza au hatuwezi kumpigia kura,” amesisitiza Al-Maliki na kuongezea kwa kusema: “sitajiondoa mpaka mwisho.”
Maliki alihudumu kama waziri mkuu wa Iraq kuanzia 2006 hadi 2014 na kama makamu wa rais kati ya 2014 na 2015 na tena kuanzia 2016 hadi 2018. Kwa sasa anaongoza harakati ya kisiasa ya Chama cha Kiislamu cha Dawa…/