
Mbunge wa kujitegemea, ambaye pia ni kiongozi wa zamani wa chama cha Leba nchini Uingereza Jeremy Corbyn, ametoa simulizi za kutisha zilizotokana na maelezo ya mkurugenzi wa Hospitali ya Al-Shifa katika Ukanda wa Ghaza uliozingirwa, zinazobainisha kwa undani jinsi utawala wa kizayuni wa Israel ulivyopeleka katika eneo hilo masanduku kadhaa yenye mafuvu ya vichwa na mabaki ya Wapalestina yaliyokatwakatwa.
Corbyn ameelezea ujumbe aliopokea kutoka kwa Dkt. Mohammed Abu Salmiya, ambaye ameripoti kwamba jeshi la Israeli lilipeleka karibu masanduku 66 ya mabaki ya binadamu kwenye kituo hicho cha tiba.
Kwa mujibu wa Corbyn, wafanyakazi wa hospitali walifungua makontena na kukuta mafuvu ya Wapalestina waliouawa wakati wa mauaji ya kimbari.
Zaidi ya hayo, kiongozi huyo wa zamani wa chama cha Leba amesema, makontena hayo yalijumuisha pia miili ya wanawake ambao mabaki yao yalikuwa na ushahidi wa mishono ya upasuaji, na kuplekea kuaminika kwamba viungo vya ndani vya maiti hao vilikuwa vimetolewa.
“Ni vigumu kulielezea hili,” amesema Corbyn na kuongeza kwamba: “Hayo ndiyo yanayowatokea watu wa Palestina. Hili ndilo piganio la zama zetu.”
Hayo yanaripotiwa huku Wizara ya Afya ya Ghaza ikiwa imethibitisha kukabidhiwa miili na mabaki kadhaa ambayo hayajatambuliwa kupitia Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC).
Maafisa wa sekta ya tiba katika eneo la tukio wameripoti kwamba, baadhi ya mabaki yalionyesha “hali zisizo za kawaida,” ikiwa ni pamoja na mikato ya upasuaji iliyoashiria kwamba viungo vilikuwa vimetolewa kabla ya miili hiyo kurudishwa Ghaza.
Dkt. Abu Salmiya, ambaye yeye mwenyewe amewahi kukamatwa na kuwekwa kizuizini na vikosi vya utawala ghasibu wa Israel, aliripoti kwamba mabaki mengi hayakuweza kutambulika, yakiwa na mifupa na mafuvu ya kichwa tu.
Wizara hiyo ya afya ya Ghaza imebainisha kuwa, miili hiyo ilipokelewa ikiwa katika “hali ya kukatwakatwa,” na kuwafanya wataalamu washindwe kuifanyia uchunguzi.
Jeremy Corbyn ameyataja mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala wa kizayuni wa Israeli huko Ghaza kuwa ni mfano sambamba wa kihistoria na mapambano ya karne ya 20 ya kupinga ufashisti…./