
Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu umekimbilia Mahakama ya Rufani katika harakati za kutaka kuingiza ushahidi mpya katika kesi hiyo.
Jamhuri imefungua shauri la maombi ya mapitio leo Jumanne Februari 24, 2026, kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuikatalia kupokea ushahidi huo mpya.
Taarifa ya kufunguliwa kwa shauri hilo imetolewa na kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka wa kesi hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Renatus Mkude.
Akijibu hoja hiyo, Lissu amesema kifungu cha 8 cha Sheria ya Mahakama ya Rufani hakiruhusu rufaa wala mapitio dhidi ya uamuzi ambao haumalizi shauri.
Amesema kuwa ingawa haombi Mahakama Kuu itoe uamuzi kwenye hilo kwa kuwa imefungwa mikono, lakini anafahamu kuwa lengo la upande wa mashtaka kufungua shauri hilo ni kurefusha shauri hilo ili yeye aendelee kukaa gerezani.
“Lengo kupeleka huko ni ili huyu mbaya wao (Lissu) aendelee kukaa gerezani. Kwa vile wanapeleka Mahakama ya Rufani napenda niseme kuwa nitawafuata huko huko nitakwenda kuwashughulikia huko huko,” amesema Lissu.
Amesema ingawa watakwenda huko Mahakama ya Rufani, anajua kuwa mwisho watarudi Mahakama Kuu awaonyeshe namna kesi hiyo ilivyo mbovu.
Kutokana na hatua hiyo, Mahakama Kuu imelazimika kusimamisha mwenendo wa kesi hiyo kwa muda usiojulikana kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika shauri hilo la mapitio.
Akitoa uamuzi wa kusimama kwa kesi hiyo, kiongozi wa jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo, Jaji Dunstan Ndunguru amesema kuwa:
“Tumesikia maombi yaliyotolewa na upande wa mashtaka na hoja za mshtakiwa, kutokana na sheria ilivyo na kama mshitakiwa alivyosema kuwa ndio utaratibu wa kisheria, mikono yetu imefungwa kwa suala hili.
“Kwa hiyo shauri hili linasimama mpaka pale shauri ambalo sasa liko Mahakama ya Rufani litakapoisha,” amesema Jaji Ndunguru
Pamoja na Jaji Ndunguru, majaji wengine katika jopo hilo ni James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kusudio la kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kesi hiyo iko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa Jamhuri na tayari mashahidi 15 kati ya 30 wanaotarajiwa wameshatoa ushahidi wao.
Jana Februari 23, 2026, upande wa mashtaka ulieleza Mahakama kuwa Februari 18, 2026 uliwasilisha mahakamani kwa njia ya mtandao, notisi ya kuongeza ushahidi katika kesi hiyo, chini ya kifungu cha 308(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga alisema katika notisi hiyo wanaomba kuongeza ushahidi mpya kwenye ushahidi wa Kamishna Msaizidi wa Polisi (ACP) Amin Mahamba kwa kuwa haukusomwa wakati wa mwenendo kabidhi, kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Katuga alisema notisi hiyo imeambatanishwa na kiini cha ushahidi huo kwamba ACP Mahamba alikuwa ni kiongozi wa timu ya upelelezi wakati uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2025 na baada ya uchaguzi.
Alibainisha kuwa ushahidi huo umetambulika kwa upande wa mashtaka wakati wa maandalizi ya shahidi huyo Februari 16, 2026.
Hata hivyo, Lissu aliibua pingamizi akidai kuwa kifungu cha 308 (1) cha CPA kilichotumiwa kinazungumzia shahidi ambaye maelezo yake hayakusomwa katika mwenendo kabidhi na si ushahidi mpya ambao haukusomwa kwenye mwenendo kabidhi.
Lissu alieleza kuwa ushahidi wa ACP Mahamba ambao Jamhuri inataka kuuongeza, ulishasomwa kwenye mwenendo kabidhi, hivyo mlango wake wa kuleta ushahidi mpya umeshafungwa.
Lissu alidai kuwa hatua ya Jamhuri kutaka kuongeza ushahidi mpya kwa kutumia shahidi ambaye tayari ushahidi wake umeshasomwa kwenye mwenendo kabidhi, ni kutaka kubadilisha hati ya mashtaka.
Hata hivyo, akijibu hoja hizo Wakili Katuga alidai kuwa kifungu cha 308 (1) cha CPA kinazungumzia notisi hiyo ya shahidi mpya au ushahidi wake ambao haukusomwa wakati wa mwenendo kabidhi.
Akijibu hoja za Wakili Katuga, Lissu alisisitiza kuwa kifungu 308 cha CPA, kinazungumzia shahidi mpya na si ushahidi mpya na kufafanua kuwa shahidi mpya ni yule ambaye maelezo au ushahidi wake hayakusomwa kwenye mwenendo kabidhi.
Alidai kutokana na kifungu hicho, ushahidi wa ACP Amini Mahamba hautoruhusiwa kwa sababu ushahidi wake ulishasomwa kwenye mwenendo kabidhi.
“Waheshimiwa majaji, mlango wa Amin Mahamba, ulishafungwa kwenye commital (mwenendo kabidhi) na kama Jamhuri wanataka maelezo hayo yazungumzwe, basi wamtafute shahidi mwingine azungumzie na si Amin Mahamba,” alidai Lissu na kusisitiza:
“Kifungu 308 kinaelekeza maelezo ya shahidi mpya ndio yanayoweza kukubaliwa, lakini kwa ushahidi wa Mahamba milango yake imefungwa na kama ukikubaliwa madhara yake ni kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka.”
Lissu alifafanua kuwa suala hilo litafumua mambo mapya na mazito yaliyotokea wakati wa uchaguzi, yakiwemo ya nani walifanya mauaji akisema kama wanataka kufanya hivyo yeye yuko tayari
Alisema tuhuma anazotuhumiwa zilifanyika Aprili 3, 2025, akashtakiwa Aprili 10, 2025 na kupelekwa mahabusu, lakini maelezo hayo ya nyongeza yanahusu masuala ya Oktoba 2025 kabla na baada ya uchaguzi.
Katika uamuzi wake Februari 24 Mahakama imekubaliana na Lissu akisema kwa mujibu wa kifungu cha 308 CPA, maelezo au ushahidi unaotolewa notisi unapaswa uwe ule ambao wakati wa mwenendo kabidhi ulikuwepo, lakini haukusomwa na si ambao haukuwepo.
“Kwa hiyo kifungu cha 308 kinafungua milango kwa shahidi ambaye maelezo yake yalikuwepo lakini hayakusomwa, lakini hakifungui mlango wa kuleta ushahidi ambao haukuwepo wala ushahidi ambao umeletwa baadaye,” amesema Jaji Ndunguru na kusisitiza:
“Notisi hii inataka kuleta ushahidi uliopatikana baada ya mwenendo kabidhi baada ya uchaguzi, hivyo ni dhahiri kwamba wakati mwenendo kabidhi unafanyika ushahidi huu haukuwepo. Hivyo inakwenda kinyume na kifungu cha 308 cha CPA,” amesema Jaji Ndunguru na kuhitimisha:
“Mahakama inakubaliana na pingamizi lililoletwa kwamba notisi hii haiendani na kifungu cha sheria na hivyo tiba pekee ni mahakama kuitupilia mbali na kwa hayo mahakama inaitupilia mbali notisi hii.
Baada ya uamuzi huo, kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili Mkude ameomba ahirisho la muda wa saa moja kutafakari uamuzi huo kabla ya kuendelea.
Lissu alipinga, akisisitiza usikilizwaji wa kesi uendelee kama ambavyo mahakama ilikuwa imeelekeza, kuwa upande wa mashtaka leo ulete mashahidi.
Hata hivyo, baada ya ufafanuzi wa Mkude kuwa hawaombi kuahirisha kesi, bali muda wa kumuandaa shahidi mambo ya kueleza kwa kuzingatia uamuzi huo, mahakama imekubali na kuahirisha kesi hiyo kwa dakika 50.
Saa tatu baadaye waendesha mashtaka waliporejea na majaji kuingia, ndipo Wakili Mkunde akaiarifu kuwa wamefungua maombi ya mapitio.
Wakili Mkude amesema anatoa taarifa hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha Sheria ya Mahakama ya Rufani Marejeo ya mwaka 2023 na Kanuni ya 65(1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani za Mwaka 2009 kama ambavyo imekuwa zikifanyiwa marekebisho.
“DPP anatoa taarifa ya kufungua maombi ya mapitio Mahakama ya Rufani dhidi ya mwenendo wa kesi hii,” amesema Wakili Mkude.
Amefafanua kuwa maombi hayo yanaungwa mkono na kiapo cha Wakili wa Serikali Cuthbert Mbilingi, kilichosainiwa Jumanne Februari 24, 2026 na kupokewa katika mifumo ya kielektoeniki na kusajiliwa kama shauri la jinai la mapitio namba 7203216/2026.