Dar es Salaam. Wakati kukiwa na sintofahamu ya ukweli wa alipo Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO), Faustine Mafwele na kile kinachozungumzwa  kwenye mitandao ya kijamii,  Kamanda wa kanda hiyo, Jumanne Muliro ametoa kauli. 

Hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii, watu waliodai kuliwakilisha kundi linalojiita Tanganyika Freedom Fighters (TFF) walichapisha ujumbe unaomuhusisha Mafwele, katika madai mbalimbali ambayo  hayajathibitishwa rasmi.

Katika ujumbe huo, watu hao walitoa kauli kali dhidi ya Mafwele wakimtuhumu kwa masuala yanayohusiana na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Akifafanua sintofahamu hiyo, Kamanda Muliro ameufananisha ujumbe wa kundi hilo kama riwaya za Shabaan Robert za kusadikika.

Amesema katika mambo ya kusadikika unaweza kusikia mtu amekufa halafu ukamuona.

Kamanda Muliro ametoa kauli hiyo alipoulizwa swali na mwandishi wa Mwananchi kuhusu ukweli wa ujumbe wa kundi hilo na alipo ZCO Mafwele.

Akijibu swali hilo,  Kamanda Muliro alianza  kwa kuelezea riwaya za Shaban Robert na kusema aliwahi kuwa na vitabu vya riwaya, moja ya vitabu hivyo  ni cha kusadikika au vitu vya kufikirika.

“Kwenye jamii kuna watu na kundi la aina hiyo na katika riwaya ile (ya Shabaan Robert) alieleza moja ya majibu ya watu wenye mtazamo wa sifa za kusadikika unaweza usiwajibu, lakini majibu baadaye watayapata wenyewe.

“Mfano wanasema mtu amekufa halafu baadaye unamuona, majibu ya swali lako (kuhusu Mafwele)  mimi hizo naziona kama riwaya, Shabaan Robert miaka ile alishaona hali hiyo ya kusadikika,” amejibu Muliro.

Madereva 250 wakamatwa

Akizungumzia hali ya usalama Dar es Salaam, Kamanda Muliro amesema jiji liko salama akibainisha kwamba kati ya Januari 30, 2026 hadi leo Februari 26 jeshi hilo kanda maalumu ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa 46 kwa makosa mbalimbali ya jinai ikiwamo unyang’anyi, uvunjaji nyumba, maghala na stoo na kuiba sambamba na wale wa kununua mali za wizi.

“Tumekamata pikipiki, simu, luninga, redio na vifaa mbalimbali vya kielektroniki,” amesema.

Mbali na watuhumiwa hao, Kamanda Muliro amesema wamewakamata pia madereva 250 ambao wamevunja sheria kwa kupita kwenye barabara za mwendokasi.

Amesema wamekamata magari 64 ambapo 45 ni ya binafsi na 19 ya Serikali pamoja na pikipiki 167  na bajaji 19 kwa kupita kwenye barabara za mwendokasi na kusababisha hatari ya mabasi ya njia hiyo na wao wenyewe.

“Wote wamechukuliwa hatua za kisheria,” amesema akisisitiza kwamba wanaendelea kutoa elimu na kuchukua hatua za kisheria kwa madereva wote wanaovunja sheria.

Akizungumzia hali ya usalama jijini Dar es Salaam amesema ni shwari akiwasisitiza wananchi kuzingatia na kufuata misingi ya sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *