
Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu sasa imehamia Mahakama ya Rufani.
Jamhuri imefungua shauri la mapitio Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, kutupilia mbali notisi yake ya kuwasilisha ushahidi mpya katika kesi hiyo.
Uamuzi huo wa Mahakama, umetolewa leo Jumanne, Februari 24, 2026 ambao ulitokana na pingamizi lililowasilishwa na Lissu, kuhusiana na taarifa ya kuongeza ushahidi wa upande wa mashtaka, iliyowasilishwa jana Jumatatu na Jamhuri.
Kutokana na hatua hiyo Mahakama Kuu kupitia kiongozi wa jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo, Dunstani Ndunguru, kama ilivyo utaratibu wa kisheria imetangaza kusimamisha usikilizwaji wa kesi hiyo mpaka Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi wa shauri hilo.
Februari 18, 2026 Jamhuri iliwasilisha taarifa hiyo mahakamani hapo chini ya kifungu 308(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai( CPA), Sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023, ikiomba mahakama kuruhusu ushahidi wa nyongeza wa shahidi wa upande wa mashtaka ambaye alikuwa kiongozi katika timu ya upelelezi, ambaye ni ACP Aman Mahamba iongezwe katika ushahidi wake wa awali.
“Kwa maoni yetu na msimamo wetu, kifungu hicho hakitoi nafasi kwa notice (taarifa) hiyo kupokewa na Mahakama na kuongezwa katika ushahidi huo,”amesema jaji Nduguru na kuongeza.
“Mahakama inaona kuwa hiyo notice (taarifa) ya kuongezwa kwa ushahidi iliyoletwa na upande wa mashtaka, haiangukii katika kifungu 308(1), hivyo Mahakama inakubaliana na pingamizi la mshtakiwa lililotolewa na haikubaliani na maombi ya upande wa Jamhuri,” amesema Jaji Ndunguru.
Endelea kufuatilia Mwananchi