MOROGORO: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sekta ya kilimo inahitaji uwekezaji wa kutosha katika mashamba makubwa, matumizi ya teknolojia za kisasa  na mitaji ya kutosha.

Profesa Mkumbo amesema hayo Februari 23,2026 wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro ya kukagua maendeleo ya uwekezaji wa kilimo eneo la Mkulazi ,tarafa ya Ngerengere mkoani humo.

Amesema kuwa kilimo kinabaki kuwa sekta muhimu ya uchumi wa taifa na ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inapaswa sekta hiyo ilindwe, itunzwe na kuendelezwe kwa ushirikiano wa dhati kati ya wananchi, serikali na wawekezaji.

Waziri Mkumbo amesema serikali itaendea kutoa  kipaumbele kwa kilimo cha kibiashara, ambacho kimejikita katika uzalishaji wa mazao ya mtama, mahindi, miwa, ufuta na alizeti.

Profesa Mkumbo amesema, licha ya kuwa na ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo, bado Tanzania inakosa tija, na sehemu kubwa ya ardhi hiyo ikiwa haijalimiwa.

Waziri Mkumbo amesema serikali imeweka miongozo ya kisera ambayo  imejikita katika kuboresha mazingira ya biashara, na bila ushirikiano wa jamii na wawekezaji, juhudi hizo zitakuwa bure.

“Tunahitaji ushirikiano wa kila mmoja bila usalama, kilimo cha kibiashara hakiwezi kustawi, wawekezaji hawa wamewekeza fedha nyingi, na kuwepo kwa  changamoto  zinapunguza tija na athari zake ni kubwa kwa uchumi wetu,” amesema Profesa  Mkumbo.

Profesa Mkumbo amesema kilimo kimekuwa sekta ya kujikimu kwa muda mrefu, na kwamba hivi sasa serikali inalenga kuhamasisha kilimo cha kibiashara, ili kuongeza uzalishaji wa mazao na kutoa ajira kwa wananchi wengi.

Amesema Serikali itaendelea kutekeleza mkakati wa kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, kwa kutoa mikopo nafuu na mafunzo kwa wakulima wadogo, huku akiwataka wawekezaji kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza uzalishaji na tija.

“Kilimo cha kisasa kinahitaji vifaa vya kisasa, mbegu bora, na mifumo ya umwagiliaji na wawekezaji hawa wanatakiwa kusaidia wakulima wadogo kwa kuwapa mafunzo na mitaji, na serikali iko tayari kutoa msaada wote unaohitajika,” amesema Profesa  Mkumbo.

Naye, Meneja Mkuu wa Santagro Ltd, Luab Luiz de Carvalho, ameiomba serikali kumalizia changamoto ya muingiliano kati yao na wafugaji ambapo wamekuwa wakiingiza mifugo shambani na kulisha mazao.

Amesema kuwa, licha ya kuwa na miundombinu imara, mifugo ni tishio kubwa kwa uwekezaji wao.

“Tunahitaji msaada wa haraka kutoka kwa serikali na jamii kuhakikisha mifugo inadhibitiwa. Bila ulinzi wa kutosha, hakuna uwekezaji wa maana utakaofaidi jamii,” amesema  de Carvalho.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mussa Kilakala, alihakikishia wawekezaji kuwa, pamoja na changamoto, wilaya  ni eneo salama la uwekezaji pamoja usalama wa maeneo ya kilimo utadumishwa kwa nguvu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *