Mexico. Kifo cha kinara wa moja ya magenge makubwa ya dawa za kulevya nchini Mexico, Nemesio Ruben Oseguera Cervantes, maarufu El Mencho, kimezua wimbi la vurugu lililoikumba nchi hiyo na kuacha hali ya hofu kwa wananchi.
Kiongozi huyo wa genge la Jalisco New Generation Cartel (CJNG), aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu na vyombo vya usalama, ameuawa juzi Jumapili, Februari 22, 2026 katika operesheni maalumu ya kijeshi iliyofanyika mji wa Tapalpa, jimboni Jalisco.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari kama Al Jazeera mara tu taarifa za kifo chake ziliposambaa, vurugu ziliripuka katika majimbo 20 kati ya 32 ya Mexico.
Video mbalimbali zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha magari yakichomwa moto, mabasi na biashara kushambuliwa, huku watu wanaodaiwa kuwa wanachama wa makundi ya uhalifu wakiweka vizuizi vya moto barabarani.
Operesheni ya kumuondoa El Mencho ilitekelezwa na vikosi maalumu vya Mexico kwa ushirikiano wa kijasusi kutoka Marekani. Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum amesema kulikuwa na ‘uratibu wa hali ya juu’ kati ya serikali ya shirikisho na majimbo yote.
Kwa upande wa Marekani, Shirika la Kudhibiti Dawa za Kulevya (DEA) lilikuwa limeweka kitita cha dola milioni 15 (sawa na Sh38.6 bilioni) kwa ambaye angefanikisha kukamatwa kwake.
Hata hivyo, mamlaka katika majimbo ya Jalisco, Michoacán na Guanajuato zimeripoti kuwa watu wasiopungua 14 waliuawa katika machafuko ya Jumapili, wakiwemo askari saba wa Kikosi cha Taifa cha Ulinzi.
Mji wa Guadalajara, mji mkuu wa Jalisco na moja ya wenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia 2026, ulikuwa kimya kwa kiasi kikubwa huku wakazi wengi wakiamua kubaki majumbani.
Kifo cha El Mencho kimeibua maswali juu ya nani atachukua nafasi yake ndani ya CJNG. Wachambuzi wa masuala ya usalama wanaeleza kuwa huenda alishateua mrithi, huku jina la mwana wa kambo wake, Juan Carlos González Valencia, likitajwa kuwa na nafasi kubwa ya kuunganisha genge hilo.
Lakini iwapo kutazuka mgawanyiko wa uongozi, wataalamu wanaonya kuwa Mexico inaweza kushuhudia ongezeko la mauaji na mapigano ya ndani kati ya makundi hasimu.
Ripoti kutoka mji mkuu, Mexico, zinaeleza kuwa migogoro ya aina hiyo imewahi kushuhudiwa katika maeneo kama Guerrero na Sinaloa, ambapo mapambano ya madaraka ndani ya magenge ya kihalifu yalisababisha kile kilichoelezwa kama vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kihalifu.
Kwa sasa, hatua ya kumuondoa El Mencho inaonekana kama ushindi mkubwa kwa serikali ya Mexico katika vita dhidi ya dawa za kulevya. Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa mafanikio hayo yanaweza kuzaa tatizo jipya ikiwa makundi ya ndani ya CJNG yataanza kugombea udhibiti.
Mexico yatuma wanajeshi 10,000 mitaani kukomesha ghasia
Taarifa ya DW inaeleza Mexico imewatuma wanajeshi 10,000 mitaani kutuliza mapigano yaliyosababishwa na mauaji ya kiongozi huyo wa kundi la CJNG.