Somaliland imeipa Marekani ofa na fursa ya kuanzisha kambi ya kijeshi katika ardhi yake. Vyanzo vya habari vimeripoti kwamba, maafisa wa Somaliland wameipa Washington ofa ya kutumia rasilimali za madini za eneo hilo na kuanzisha kambi ya kijeshi.

Khadir Hussein Abdi, Waziri wa Ofisi ya Rais wa Somaliland, amesema kuhusiana na hili: “Tuko tayari kuipa Marekani fursa ya kuhodhi ufikiaji wa madini na kuanzisha ya kambi za kijeshi.” Aliongeza kuwa, pendekezo hili linalenga kusukuma mbele gurudumu la kukubalika kimataifa.

Pendekezo hili linakuja huku utawala vamizi wa Israel ulilitambua eneo la Somaliland kama nchi huru mnamo Desemba 2025, hatua iliyofuatiwa na radiamali za kikanda na kimataifa. Mataifa ya Misri, Jordan, Djibouti, Saudi Arabia, na Uturuki, na nchi 20 za Asia Magharibi na Afrika yamelaani kitendo hiki cha Israel katika taarifa ya pamoja. Wakati huo huo, hatua za serikali ya shirikisho ya Somalia za kuzuia utekelezaji wa mipango hatari ya Israel huko Somaliland si tu ni jibu kwa harakati za eneo hili linalotaka kujitenga, lakini pia ni sehemu ya mkakati mpana wa kudumisha umoja wa kitaifa, kuzuia uingiliaji wa kigeni, na kuimarisha serikali kuu katika mojawapo ya maeneo nyeti zaidi barani Afrika.

Filihali eneo lililojitangazia mamlaka ya ndani la Somaliland linaonekana kufanya jaribio jipya la kupata usaidizi na kutambuliwa kimataifa kwa kuipa Marekani kambi ya kijeshi na ufikiaji wa kipekee wa rasilimali zake za madini. Hii inakuja licha ya ukweli kwamba Somaliland ambayo ilitangaza uhuru wake mwaka wa 1991 bado haijtambuliwa kama sehemu ya Somalia na jamii ya kimataifa na serikali ya shirikisho.

Sababu kuu za pendekezo hili zinaweza kufuatiliwa kutokana na mambo kadhaa muhimu. Sababu ya kwanza na muhimu zaidi ni jaribio la kutaka kuondoka katika hali ya kutengwa kidiplomasia. Licha ya kuwa na serikali huru, jeshi, na sarafu, lakini Somaliland imeshindwa kupata uhalali na kutambuliwa kimataifa kwa miongo mitatu iliyopita. Ofa hii kwa Marekani kwa kweli ni mwendelezo wa mchakato ulioanza Desemba 2025 kwa kutambuliwa na Israel. Maafisa wa Somaliland wanatumai kwamba, kwa kuwa mshirika wa kimkakati wa Washington, wataweza kuvutia maoni chanya ya mataifa mengine yenye nguvu duniani.

Sababu ya pili ni umuhimuu na unyeti mkubwa wa kisiasa la eneo hilo. Somaliland iko kwenye mwambao wa Ghuba ya Aden, mkabala kabisa na Yemen. Kwa kuzingatia mashambulizi ya mara kwa mara ya muqawama wa Yemen dhidi ya meli zinazohusiana na utawala wa Kizayuni katika njia hii muhimu ya maji, kuwa na kambi kwenye mwambao wa kusini wa Ghuba ya Aden kuna thamani kubwa ya kijeshi na kiusalama kwa Marekani na washirika wake. Eneo hili linaweza kutumika kama sehemu ya ufuatiliaji na majibu ya haraka kwa matukio nchini Yemen na kuhakikisha usalama wa njia za meli, bila shaka, sambamba na maslahi ya Magharibi na Tel Aviv.

Sababu ya tatu ni utajiri na rasilimali za madini zilizotangazwa katika eneo hilo. Maafisa wa Somaliland wanadai kuweko akiba kubwa ya madini muhimu kama vile lithiamu na koltani, ambayo ni muhimu kwa sekta zilizoendelea na za ulinzi duniani. Ingawa tafiti huru bado hazijathibitisha kiwango halisi cha akiba hizi, lakini uwezo huu pia umetumika kama njia yenye nguvu ya kuvutia umakini wa Marekani.

Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, pendekezo hili linaweza kuwa na athari kadhaa. Kwa upande mmoja, makubaliano yoyote ya kijeshi kati ya Marekani na Somaliland yataathiri vibaya uhusiano wa Marekani na serikali ya shirikisho ya Somalia. Maafisa wa Somalia hapo awali walitaka ushirikiano wa kijeshi ndani ya mfumo wa kisheria na kupitia serikali kuu, wakitaja makubaliano ya zamani ya 1980, na wanaona makubaliano yoyote tofauti na hayo kuwa ni kinyume na uhuru wao.

Kwa upande mwingine, hatua hii inaweza kuibua mvutano ulioongezeka katika eneo hilo. Na mwisho ni kuwa, ingawa serikali ya Marekani bado haijatangaza msimamo rasmi, na Donald Trump pia amekataa uwezekano wa kuitambua Somaliland, lakini pendekezo hili linaonyesha mabadiliko katika milingano ya nguvu na ushindani wa ushawishi katika eneo la Pembe ya Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *