
Dar es Salaam. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, imetupilia mbali ushahidi mpya wa Jamhuri, ikieleza kuwa kifungu kilichotumika kuwasilisha taarifa ya kuongeza ushahidi wanyongeza hakitoi nafasi kwa taarifa hiyo kupokewa na kuongezwa katika ushahidi huo.
Uamuzi huo unatokana na pingamizi liliwasilishwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu, kuhusiana na taarifa ya kuongeza ushahidi wa upande wa mashtaka, iliyowasilishwa na Jamhuri.
Februari 18, 2026 Jamhuri iliwasilisha taarifa hiyo mahakamani hapo chini ya kifungu 308(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai( CPA), Sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023, ikiomba mahakama kuruhusu ushahidi wa nyongeza wa shahidi wa upande wa mashtaka ambaye alikuwa kiongozi katika timu ya upelelezi, ambaye ni ACP Aman Mahamba iongezwe katika ushahidi wake wa awali.
Katika uamuzi wa Mahakama, uliotolewa leo Jumanne Februari 24, 2026 na Jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, umeeleza kuwa kifungu kilichotumika hakitoi nafasi ya kuleta taarifa ya kuongeza ushahidi.
“Kwa maoni yetu na msimamo wetu, kifungu hicho hakitoi nafasi kwa notice (taarifa) hiyo kupokewa na Mahakama na kuongezwa katika ushahidi huo,”amesema jaji Nduguru na kuongeza.
“Mahakama inaona kuwa hiyo notise ( taarifa) ya kuongezwa kwa ushahidi iliyoletwa na upande wa mashtaka, haiangukii katika kifungu 308(1), hivyo Mahakama inakubaliana na pingamizi la mshtakiwa lililotolewa na haikubaliani na maombi ya upande wa Jamhuri,” amesema Jaji Ndunguru.
Baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, kiongozi wa Jopo la mawakili wa Serikali, Wakili Mkuu wa Serikali, Renatus Mkude, ameiomba Mahakama itoe ahirisho la saa moja ili waende kutafakari uamuzi huo na kisha watarejea kuendelea na kesi.
Hata hivyo, Mahakama imekubaliana na ombi hilo na imeahirisha kesi kwa dakika 50.