DODOMA: Rais wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dk Samia Suluhu Hassan, amesema jengo jipya la Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa jijini Dodoma ni alama ya ukomavu wa taifa na uthibitisho wa uwezo wa Watanzania kupanga, kuamua na kutekeleza miradi mikubwa kwa kutumia rasilimali na wataalamu wa ndani.

Akizungumza leo Februari 24, 2026 katika uzinduzi wa jengo hilo uliofanyika jijini Dodoma, Rais Samia amesema uwekezaji huo unaimarisha uhuru wa maamuzi ya taifa na kulipa heshima katika masuala ya ulinzi Afrika, akibainisha kuwa Tanzania sasa ni miongoni mwa nchi zilizotoa kipaumbele cha juu kwa shughuli za ulinzi.

Hata hivyo, ameonya kuwa majengo hayo yasibaki kuwa fahari ya muonekano pekee, bali yatumike kikamilifu kuimarisha usimamizi wa ulinzi wa taifa.


Alisisitiza kuwa makao makuu hayo yanapaswa kuwa kituo cha fikra, uchambuzi wa kitaalamu na uratibu wa kisayansi wa mikakati ya ulinzi inayoendana na mabadiliko ya wakati.

Rais Samia ameeleza kuwa katika mazingira ya sasa ya usalama wa dunia, ulinzi hauhusiani na silaha pekee, bali unategemea pia upatikanaji na uchambuzi wa taarifa, matumizi ya teknolojia za kisasa, mifumo madhubuti ya mawasiliano pamoja na ubobezi wa hali ya juu wa kitaalamu.

Amebainisha kuwa baada ya kulitembelea jengo hilo, ameridhishwa na hatua zilizofikiwa katika kuzingatia matumizi ya teknolojia na mifumo ya kisasa, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza nguvu katika awamu zijazo za ujenzi.

Rais Samia, ameahidi kuhakikisha kuwa awamu zilizobaki za mradi huo zinakamilishwa kwa wakati, ili kuendelea kuimarisha uwezo wa taifa katika kulinda mipaka, maslahi na usalama wa nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *