Dar es Salaam. Mwenyekiti mpya wa Chama cha Wananchi (CUF), Mirambo Yusuf, amesema anaandaa utaratibu wa haraka kukutana na mtangulizi wake, Profesa Ibrahim Lipumba, kwa mazungumzo ya kina kabla ya kukabidhiana ofisi rasmi.

Mirambo alichaguliwa kushika wadhifa huo na kuwa Mwenyekiti wa nne tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1992, katika Mkutano Mkuu uliofanyika Februari 22, 2026, katika Ukumbi wa Lekham, Buguruni, jijini Dar es Salaam.

Amechukua madaraka katika kipindi ambacho wanachama wa chama hicho wamegawanyika katika makundi mawili kufuatia uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa uliotolewa Februari 13, 2026, uliotengua uongozi uliomweka madarakani Profesa Lipumba na wenzake.

Kwa mujibu wa Msajili, msingi wa kutengua uchaguzi huo ni kwamba Profesa Lipumba na wenzake hawakuvuka nusu ya kura halali zilizopigwa katika uchaguzi uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024.

Hivyo, kwa kuzingatia kanuni na matakwa ya Katiba ya chama ya mwaka 1992 pamoja na marekebisho ya mwaka 2014, mchakato huo ulipaswa kurudiwa.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Februari 24, 2026 Mirambo amesema licha ya kuchukua madaraka katika mazingira ambayo huenda hayakumpendeza mtangulizi wake, yupo tayari kumuita kwa mazungumzo ya kina na kundi lake kabla ya kukabidhiana ofisi, ambazo Lipumba alizishikilia kwa miaka 27.

“Nipo katika hatua za mwisho za kumuita ili tuzungumze, na kundi lake kwa kuwa yeye ni mtangulizi wangu. Lakini kama unavyojua, bado hatujakabidhiana ofisi, nahitaji kujifunza mengi lakini kuunganisha hiki chama tuondokane na migogoro” amesema.

Amesema Lipumba hakuondoshwa madarakani na kundi lake  kwa hila kama uvumi unavyoenea, bali aliondolewa kwa kuzingatia kanuni na vifungu vya Katiba, baada ya baadhi ya wanachama kuwasilisha malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

Amesema wamepanga kukutana kuanzia wiki ijayo katika makao makuu ya chama hicho, huku akisisitiza kuwa ataendelea kumheshimu na kumtumia kama mshauri kutokana na uzoefu wake wa uongozi.

“Namuheshimu Profesa Lipumba; ni kiongozi na mwalimu wangu wa siasa. Nimekuwa chini ya uongozi wake kwa miaka 10 nikiwa Mwenyekiti wa chama Wilaya ya Tabora, hivyo namfahamu na ninaelewa misimamo yake. Natafuta muda ili tukutane tuzungumze,” amesema.

Amesema baada ya Profesa Lipumba kurejea madarakani mwaka 2024, hakuwa sehemu ya uongozi wake kwani alikuwa mwanachama wa kawaida.

“Bado namtegemea kunishauri namna ya kumaliza migogoro ya kiuongozi na kifedha inayokikabili chama, kwa sababu hatuna ruzuku na ni lazima chama kijiendeshe kama taasisi imara nyakati zote,” amesema.

Mirambo amesema wakati wa kampeni aliahidi kujenga umoja ndani ya chama na kukifanya kiaminike ili kuvutia wafadhili wenye uwezo wa kifedha.

“Chama hakiwezi kupiga hatua kwa kutegemea michango ya kadi za wanachama pekee. Lazima tuwe na vyanzo vingine mbadala kwa maslahi ya ustawi wa chama chetu na kuondokana na mpito tunaoupitia,” amesema.

Baada ya kuingia madarakani Februari 21, 2026, siku iliyofuata alimteua Katibu Mkuu, Hamad Masoud Hamad, pamoja na viongozi wengine wachache, huku akiacha wazi nafasi za Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.

Alipoulizwa kwa nini hajafanya uteuzi katika nafasi hizo muhimu, Mirambo amesema uchaguzi huo ulikuwa wa ghafla, hivyo aliamua kuanza na uteuzi wa Katibu Mkuu huku akiendelea kufanya tathmini ya kina kwa nafasi zilizobaki.

Wakati akieleza hayo, upande unaopinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, ukiongozwa na Magdalena Sakaya, umesema tayari umefungua shauri mahakamani kupinga hatua zilizochukuliwa na Msajili.

“Tayari tumeshafungua shauri tangu Februari 20; tunachosubiri ni kupangiwa siku ya kusikilizwa. Hatujakubaliana na hatua zilizochukuliwa na Msajili, tunataka haki itendeke,” amesema.

Sakaya amesema uamuzi wa Msajili haukuzingatia haki za msingi, ikiwemo wao kupewa nafasi ya kusikilizwa dhidi ya madai yaliyowasilishwa na walalamikaji.

Jitihada za kumpata Profesa Lipumba zinaendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *