Mwigulu: Hakuna mwenye haki kuliko mwingineMwigulu: Hakuna mwenye haki kuliko mwingine

WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema Tanzania ni nchi ya wote na hakuna mwenye haki kuliko mwingine.

Dk Mwigulu alisema hayo wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara Ngaramtoni mkoani Arusha.

“Tanzania ni nchi ya wote, isitokee kwamba mtu akiwa na fedha yeye ni Mtanzania na nusu na aliye masikini ndio Mtanzania. Watanzania wote wana haki sawa,” alisema Dk Mwigulu.

Dk Mwigulu alikemea watumishi wazembe na akasema serikali haikupeleka watumishi katika maeneo ya kiutawala ili wagawane vyeo.

SOMA: Mwigulu: Watendaji msizoee shida za wananchi

“Kumetokea na tabia ya watu kujali mambo yao binafsi tu, mwananchi anakuwa na kero hadi amuone mkuu wa wilaya wewe ulioko kwenye kijiji, kata upo wapi, hivi ndivyo muundo wetu wa utawala unataka tufanye kazi?” alihoji.

Aliongeza: “Watu wanathamini mambo yao binafsi na umbea, kwenye umbea utawasikia, hoja za watu wanaacha washughulike nazo wao wenyewe huu sio utaratibu na makusudi ya muundo wetu wa serikali”.

Waziri Mkuu ameagiza kila mtendaji wa serikali katika maeneo yake awe na jedwali linaloonesha kero anazozipokea na namna wanavyozishughulikia pamoja na kuchukua hatua za haraka kwa kufanya ufumbuzi wa changamoto husika.

“Kumekuwepo na kupuuza mtu anayefika kueleza kero yake kwa serikali na wakati mwingine serikali mnatambua kabisa huyu kaonewa na ana haki katika suala hilo halafu mnamuacha mbabe anaendelea kutamba tu huku tuna vyombo vya dola,” alisema Dk Mwigulu.

“Sehemu nyingine mahakama inasema mwenye haki ni huyu hapa mbabe mmoja anakataa tu na dola ipo. Wale watu wasioheshimu wenzao kwa ubabe wanatumia mtaji wa mnyonge, wao wanakipato au wanamtandao washikisheni adabu,” aliongeza.

Alibainisha kuwa wakati akiendelea na ziara hiyo amegundua baadhi ya maeneo serikali inalaumiwa kwa sababu ya watumishi wavivu na wazembe.

“Hatuwezi tukawa na watu wa kupuuza mambo ya msingi yanayowahusu wananchi wenzao. Nimegundua tabia ya kupuuza kero za watu imeendelea kushamiri mtu anapewa tenda ya ujenzi wa mradi, serikali inamlipa anamaliza mradi wale aliyowapa mikataba midogo hajawalipa pengine wengine wanaodai wanadhani serikali haijawalipa. Nimeagiza ifanyike tathmini watakaobainika walifanya hivyo wasipewe mradi wowote hapa nchini,” aliagiza.

Alisema anaona fahari kuona miradi ya maendeleo ikizinduliwa kwa sababu ni kazi zinazoleta heshima kwa
nchi huru na inayoendelea kama Tanzania na zinatafsiri maana ya utu na ni maono ya Rais Samia Suluhu Hassan
ya kubadilisha maisha ya Watanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *