
Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina imesema uwekezaji wa Serikali katika kampuni ambazo inamiliki hisa chache (chini ya asilimia 51) umeleta faida ya kifedha pamoja na kuongeza ajira kwa Watanzania.
Katika kipindi cha miaka minne (2020–2024), thamani ya uwekezaji huo imeongezeka kutoka Sh821.5 bilioni hadi Sh1.94 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 136. Mapato ghafi yameongezeka kutoka Sh6.81 trilioni hadi Sh10.74 trilioni (asilimia 58), huku faida ikipanda kutoka Sh1.79 trilioni hadi Sh1.95 trilioni. Kampuni hizo pia zimechangia takribani Sh3.67 trilioni kama kodi ya mapato ya kampuni katika kipindi hicho.
Aidha, gawio kwa Serikali limeongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka Sh58.26 bilioni mwaka 2021 hadi Sh266.52 bilioni kufikia Juni 30, 2025, sawa na ongezeko la asilimia 357.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma, Sura ya 257, taasisi ambazo Serikali inamiliki asilimia 51 au zaidi hutambuliwa kama mashirika au taasisi za umma. Hadi Juni 30, 2025 kulikuwa na Taasisi za Umma 252 na kampuni 56 zenye hisa chache, jumla ya taasisi 308 zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Akizungumza Dar es Salaam kuhusu mkutano wa jukwaa la wakurugenzi wa bodi na watendaji wakuu wa kampuni ambazo Serikali ina hisa chache (Minority Interest Forum–MIF 2026), Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Mashirika ya Kibiashara, Lightness Mauki, amesema kampuni hizo zimekuwa chachu ya ukuaji wa uchumi kwa kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na gawio, kukuza ajira na ujuzi wa Watanzania, pamoja na kuchangia sekta za benki, madini, nishati, mawasiliano na viwanda.
Kwa upande wake, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano, amesema mmiliki wa kampuni anapaswa kufaidika na uwekezaji wake endapo kampuni inaendeshwa kwa ufanisi na faida. Ameongeza kuwa pamoja na umuhimu wa kuongeza uwekezaji, kipaumbele kinapaswa kuwa katika ufanisi wa uendeshaji ili matokeo yaonekane katika ajira, mapato ya kodi, ubora wa huduma na gawio. Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ufanisi wa mashirika ya umma, hususan yale ambayo Serikali inamiliki zaidi ya asilimia 50 au 100.
Kuhusu mkutano wa Arusha
Mkutano wa MIF 2026 utafanyika Machi 16–18, 2026 jijini Arusha. Lengo lake ni kuimarisha uwezo wa wakurugenzi wa bodi wa kampuni ambazo Serikali ina hisa chache ili waweze kuongoza kwa mtazamo wa kimkakati, bunifu na unaoendana na mabadiliko ya soko na teknolojia.
Kwa mujibu wa Mauki, mkutano huo unalenga kuhamasisha mabadiliko kutoka ufuatiliaji wa kawaida wa utendaji (oversight) kwenda uongozi unaotazama mbele (foresight), unaotambua vihatarishi na fursa mapema, na unaojibu haraka mabadiliko ya kiuchumi na kibiashara. Mada zitakazojadiliwa ni pamoja na utawala unaotambua vihatarishi vinavyoibuka, ubunifu na ushindani endelevu, athari za siasa na uchumi wa kimataifa, usalama wa mitandao (cybersecurity) na mtikisiko wa soko.
Huu ni mkutano wa tatu tangu kuanzishwa kwa jukwaa hilo, ukitarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya wakurugenzi wa bodi na watendaji wakuu 150 kutoka kampuni 56. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji.