Dar es Salaam. Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amesema mamlaka hiyo inaimarisha mifumo yake ya teknolojia kuwabaini vigogo wanaofadhili biashara ya dawa za kulevya.

Amesema teknolojia hiyo, itawezesha kuwabaini kwa njia rahisi hata vigogo wenye nyadhifa mbalimbali ili wakamatwe na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Tayari maofisa wa DCEA wanapata mafunzo nje ya nchi kuendesha mfumo huo wa teknolojia kuwabaini wote wanaohusika kwenye mnyororo wa biashara hiyo haramu.

Uamuzi wa mamlaka hiyo, unatokana na kile kilichoelezwa na Lyimo kuwa, biashara ya dawa za kulevya, ukiacha wafanyabiashara wakubwa wanaouza na wale wadogo wanaosambaza, pia huwa na wafadhili ambao mara nyingi ni vigumu kuonekana.

Lyimo ameeleza hayo wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika katika ofisi za mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.

Amesema mtandao wa biashara za dawa za kulevya unahusisha wafanyabiashara wakubwa wanaouza, wale wa kati wanaotumika kusambaza, kadhalika kuna wanaofadhili na hao mara nyingi ni vigumu kujulikana.

Ameeleza wafadhili wa dawa hizo, huwa vigumu kukutana naye moja kwa moja, bali hukutana na wafanyabiashara wanaopokea ufadhili na wale wadogo wanaosambaza dawa.

“Kuhakikisha tunakabiliana na hilo, kwa sababu wale wadogo na wakubwa tumeshawakamata, hawa wanaofadhili lazima kuwe na mbinu za kidijitali kuwakamata,” amesema.

Ameeleza wafadhili hao huwa hawagusi dawa na DCEA ipo kwenye maandalizi ya kuanzisha kitengo kitachohusisha matumizi ya sayansi na teknolojia kuwanasa wote wanaohusika kwenye mnyororo wa biashara ya dawa za kulevya, wakiwamo wale wanaofadhili ambao awali ilikuwa vigumu kutoa ushahidi wa kuwatia hatiani.

“Lazima tukuunganishe kidijitali, kiteknolojia wewe unahusika vipi na huyu mtu mkubwa tuliyemkamata wa dawa za kulevya,” amesema.

Amesema teknolojia hiyo inafanywa kuhakikisha bila kujali ukubwa au wadhifa ulionao, unaunganishwa na hatimaye kubainika na kukamatwa.

“Tutahakikisha kama kuna mtu yeyote mkubwa ambaye anajiita mkubwa wao, kwa sababu kwenye sheria hakuna mkubwa, hata kama una nafasi gani tutakukamata.

“Hili tunaliimarisha na kuna maofisa tumewateua watapata mafunzo maalumu kwa ajili ya kusimamia kitengo cha Forensic,” amesema.

Ameeleza kama kuna mtu yeyote anayefadhili biashara bila kujali wadhifa au umaarufu wake, ajiandae muda wowote atakamatwa kwa kuwa, DCEA ina mamlaka ya kumkamata yeyote ilimradi kuwe na ushahidi wa kuhusika kwake.

“Sidhani kama kuna mtu atapona kwenye hilo, tunahakikisha hili tunalisimamia kwa nguvu zote kuhakikisha tunalifanikisha mapema na hicho kitengo kinakamilika mapema,” amesema.

Walivyomaliza mateja

Akizungumzia hilo, Lyimo amesema miaka mitatu nyuma karibu katika kila kituo cha daladala na baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam kulijaa waraibu wa dawa za kulevya maarufu ‘mateja.’

Ameyataja maeneo yaliyokuwa na waraibu hao ni Mwenge, Makumbusho, Mwananyamala, Kinondoni, Manzese na Kwa Mfuga Mbwa.

Amesema wingi wa mateja uliambatana na wingi wa matukio ya kihalifu, kwa nyakati hizo, isingekuwa rahisi kutembea na cheni, pete na kitu chochote cha thamani bila kuporwa, ama kwa kupigwa roba au kunyang’anywa.

“Walivyokuwa wengi walikuwa wanapora kwa nguvu muda wowote, kutokana na kwamba ni waathiriwa wa dawa za kulevya,” amesema.

Lakini, amesema hali imekuwa tofauti kwa sasa, kwa kuwa, ‘mateja’ wamepungua na wengi wapo kliniki za matibabu na hospitali kadhaa za umma, wakipatiwa matibabu ya bure, kwa gharama za Serikali.

Amesema kilichojificha nyuma ya kupungua kwa ‘mateja’ ni operesheni mbalimbali zinazofanywa na DCEA kuhakikisha dawa za kulevya zinapungua mitaani.

Lyimo ameeleza kuwa si rahisi kushuhudia mtu akisaga dawa za kulevya na kuvuta, au kuwashuhudia ‘mateja’ wengi barabarani, lakini oparesheni za mtaa kwa mtaa, pori kwa pori, nyumba kwa nyumba na shamba kwa shamba zimekomesha hilo.

“Operesheni hii imefanyika kwa ukubwa. Kwa kipindi cha hii miaka mitatu pekee, dawa za kulevya kilogramu milioni 5.4 zimekamatwa, hizi ni nyingi sana ni kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika historia ya Tanzania,” amesema Lyimo.

Baada ya kupungua kwa dawa za kulevya nchini, amesema Serikali ikaanza kazi ya kujenga kliniki za matibabu kwa waraibu ambazo kwa sasa zimefika 21 na nyumba za upataji nafuu yaani soba, zimefika 77.

“Watu baada ya kukosa dawa za kulevya wakawa wanahitaji zaidi matibabu ndio maana tukajenga hizo nyumba za upataji nafuu na kliniki za matibabu,” amesema Lyimo.

Walivyomaliza Heroine na Cocaine

Lyimo, amesema hatua ya kupungua kwa dawa za kulevya nchini hasa Heroine na Cocaine, imetokana na kukamatwa kwa mitandao mikubwa ya vigogo wa uuzaji wa dawa hizo.

Kwa kipindi cha miaka mitatu, amesema mitandao 10 ya wauzaji wa dawa za kulevya imekamatwa, hiyo inawahusisha waliokuwepo ndani na nje ya nchi.

“Ukizungumzia Cocaine huo ni mtandao mmoja wa dawa za kulevya…kulikuwa na vigogo waliopo Tanzania kazi yao ni kusambaza na kuzipokea, kulikuwa na wengine nje ya nchi, kazi yao kuziingiza Tanzania.

“Kuna ambao wako hapa kazi yao wanazifunga na kumezesha watu kwenye matumbo na wanazisafirisha kwenye maeneo mbalimbali duniani, unapomaliza hiyo, huo ndio mtandao mmoja kwa hiyo fikiria unapomaliza mitandao 10 unakuwa umepunguza kiasi gani,” amesema Lyimo.

Amesema kulikuwa na mitandao ya Cocaine, skanka, bangi, dawa tiba zenye asili ya kulevya, kemikali bashirifu zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya na dawa aina mbalimbali.

Amesema mtandao mkubwa uliomaliza siku za karibuni ni wa dawa mpya aina ya Mitragyna speciose uliokuwa na wadau kutoka ndani na nje ya nchi na tani 30 zilikamatwa.

Mtandao huo pekee, amesema ulikuwa na wafanyabiashara kutoka Sri Lanka, Dubai na India wote kwa ajili ya kusambaza dawa hizo ndani na nje ya nchi.

“Tumekamata hata wale waliokuwa wanasambaza nje ya nchi kwa maana waliokuwa Sri Lanka. Hata, mtandao wa Heroine tumekamata watu wa Nigeria na mataifa mengine waliokuwa wanasambaza,” amesema.

Ameeleza mapapa wote wa dawa za kulevya waliokamatwa wapo katika Mahakama za mafisadi kwa hatua za kisheria na wamehifadhiwa kwenye mahabusu maalumu.

Ili kuwakamata wale walioko nje ya nchi, amesema kuna ushirikiano na mataifa mbalimbali, hivyo wakibaini mtandao unaohusisha waliopo nje wanawasiliana na nchi husika kwa hatua za ukamataji.

“Mfano mtandao wa Heroine ulikuwa na watu kutoka Afrika Kusini, Nigeria, Tanzania na nchi za Asia. Wale wa Asia tumewakamata hapa Tanzania, wale wa Afrika Kusini tumewasiliana na nchi zao na tumewakamata na wale wa Nigeria tumetumia mbinu za operesheni tumewakamata wakiwa nchini kuangalia biashara zao,” amesema.

Lyimo amesema wakati mwingine, wanatumia Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Uhalifu Duniani linatumika kuiunganisha DCEA na nchi mbalimbali ambazo wahalifu hao wanapatikana.

Pia, amesema wanashirikiana na Interpol ambayo imefunga vifaa vyao nchini na wanawasiliana nao kwa njia ya kidijitali na akitokea mhusika wanatoa taarifa zao na kuwakamata.

Ameeleza kwa sasa Serikali imewakusanya waraibu wa dawa za kulevya na kuanzisha taasisi zisizo za Serikali kuwasajili waraibu na kuwapeleka kwenye matibabu ili wapone na warudi katika hali zao.

Hilo limeambatana na kile alichosema, Serikali imetoa kibali kuziruhusu hospitali zote za umma kuwatibu waraibu wa dawa hizo na kwa miaka mitatu waraibu 900,000 wameshapata huduma.

Kwa upande wa kliniki kwa sasa zimefika zaidi ya 21 na nyumba za upataji nafuu 77 na zaidi ya watu milioni moja wameshapatiwa matibabu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *