LEO jioni kikosi cha Yanga kitashuka kwenye uwanja wa nyumbani wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam kuvaana na JKT Tanzania, huku kikitimiza siku 476 katika Ligi Kuu Bara ikicheza mechi 29 bila kupoteza (unbeaten).

Mara ya mwisho kwa Yanga kuonja kipigo katika ligi ilikuwa Novemba 7, 2024 ilipofumuliwa mabao 3-1 na Tabora United (sasa TRA United) kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, ikiwa ni siku chache tu tangu ilipolazwa bao 1-0 na Azam na kutibuliwa rekodi iliyokuwa nayo kipindi hicho.

Kabla ya kipigo cha Azam, watetezi hao wa ligi walikuwa wamecheza mechi nane mfululizo bila kupoteza wala kuruhusu bao, lakini Wanalambalamba wakawatibulia na Tabora United ikaja kuongeza mumivu kwa kipigo hicho kizito cha mabao 3-1.

Hata hivyo, mara baada ya kipigo hicho ni kama vile Yanga ilizinduka usingizini na kupambana kwa kutoa dozi hadi kumaliza msimu huo 2024-2025 ikitetea taji kwa mara nne mfululizo na kuendeleza moto huo msimu huu, kwani ushindi ilioupata Jumapili iliyopita dhidi ya Namungo ulikuwa ni wa 27 katika mechi 29 za Ligi Kuu Bara ilizocheza tangu ilipopoteza mara ya mwisho mbele ya Nyuki wa Tabora.

Kipigo hicho cha mwisho kilihitimisha safari ya Kocha Miguel Gamondi ndani ya Yanga ambaye kwa sasa anainoa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, iliyomchukua kutoka Singida Black Stars.

Ubabe huo wa Yanga kutofungwa jumla ya mechi 29, mbili kati ya  hizo ilitoka suluhu dhidi ya JKT Tanzania Februari 10, 2025 msimu uliopita 2024-2025 na dhidi ya Mbeya City, Septemba 30, 2025 msimu huu wa 2025-2026.

Msimu wa 2024-2025 katika mechi 20, Yanga ilifunga mabao 74, iliruhusu matano, cleansheets zilikuwa 15, huku msimu wa 2025-2026 katika mechi tisa imefunga mabao 21, imeruhusu mawili na cleasheets saba, hivyo wastani wa kufunga ni mabao 3.28 kwa mechi na wastani wa kuruhusu bao ni 0.24 kwa mechi.

Katika mechi ambazo zilikuwa na mabao mengi ni; Yanga 6-1 KenGold, KMC 1-6 Yanga, Yanga 6-0 Mashujaa, Yanga 5-0 Fountain Gate, Yanga 5-0 Dodoma, Tanzania Prisons 0-5 Yanga na Mashujaa 0-5 Yanga.

Takwimu zingine zinaonyesha Yanga imefunga mabao 34 nyumbani na imeruhusu mawili, ina wastani wa kufunga mabao 4.85 kwa mechi, wakati ugenini imefunga mabao 24 na kuruhusu moja.

Tangu Novemba 7, 2024 hadi leo Februari 25, 2026 inapokwenda kucheza dhidi ya JKT Tanzania, ni sawa na siku 476 zimepita tangu Yanga ipoteze mechi ya Ligi Kuu Bara, ikiwa ni sawa na mwaka mmoja, miezi mitatu na siku 19.

Kutokana na kiwango kilichoonyesha Yanga, kimechambuliwa na watalamu wa soka hapa nchini, wakisema uwekezaji katika usajili ni mojawapo ya sababu ya mafanikio hayo.

Miongoni mwa waliotoa maoni yao ni staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella, aliyesema: “Yanga ina wachezaji wenye viwango vya juu kwa miaka ya hivi karibuni, ndiyo maana timu inashinda na hairuhusu mabao mengi, pia kuwa upande wa viongozi kuna utulivu unaowasaidia kufanya kazi kwa umoja.”

Mchezaji mwingine wa zamani wa Simba na Yanga, Amir Maftah alisema:

“Kinachoibeba Yanga ni ubora wa kikosi chake, inafunga na hairuhusu sana mabao, ukiachana na hilo ndiyo maana imechukua ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo.”

Kwa upande wa kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni, alisema: “Soka linachezwa kwa wazi, Yanga ina wachezaji wazuri, hilo linaonyesha uwekezaji wa usajili waliyoufanya.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *