• Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, amewashukuru Wakenya kwa kumuunga mkono katika mikutano ya Linda Mwananchi iliyofanyika katika maeneo manne
  • Sifuna aliwahimiza vijana kuleta mabadiliko ya kisiasa na kujitokeza kugombea nyadhifa mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa 2027
  • Pia alisimulia kuhusu simu muhimu aliyopokea kutoka kwa rafiki wa mamake baada ya tukio la kurushiwa vitoa machozi katika mkutano wa Kakamega

Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, amewashukuru Wakenya kwa kujitokeza kwa wingi kuunga mkono mikutano ya Linda Mwananchi.

Edwin Sifuna akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Linda Mwananchi mjini Kakamega.
Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna afichua mazungumzo yake na rafikiye mamake baada ya mkutano mkubwa wa Kakamega. Picha: Edwin Sifuna.
Source: Facebook

Mikutano hiyo ilianzishwa na baadhi ya wanachama wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) waliotajwa kama waasi, akiwemo aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Mbunge wa Embakasi Babu Owino, na Gavana wa Siaya James Orengo, miongoni mwa wabunge wengine.

Sifuna aliwapa ujumbe gani vijana?

Akizungumza katika mahojiano kwenye NTV Jumanne, Februari 24, Sifuna alisema alivutiwa na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kwenye mikutano hiyo.

Anaamini kuwa uungwaji mkono huo unaonyesha utayari wa Wakenya kuendeleza ajenda na sera zake licha ya mashambulizi yoyote.

Pia soma

James Orengo Aonya Dhidi ya Kusambaratisha Mkutano wa Linda Mwananchi Huko Kakamega: “Ni Tsunami”

“Nimeshangazwa na wingi wa uungwaji mkono kutoka kwa Wakenya wa tabaka zote za maisha, na nachukua fursa hii kuwashukuru. Inatia faraja kubwa kujua kwamba hauko peke yako. Inatia faraja kujua kwamba iwapo jambo lolote lingetokea kwangu, kuna Sifuna wengine huko nje. Nimehisi upendo na uungwaji mkono,” alisema.

Hata hivyo, Sifuna aliwaonya Wakenya dhidi ya kumlaumu kwa kila kosa licha ya kukiri kuwa wengi wanajitambulisha na sera zake na changamoto alizokumbana nazo ndani ya ODM.

“Ninaomba wasitumie jina langu kwa kila kitu halafu nalaumiwa. Sisi ni binadamu wenye mapungufu makubwa. Hatujakamilika. Nitajaribu kadri niwezavyo kutomwangusha yeyote,” aliapa.

Mwanasiasa huyo aliwahimiza zaidi vijana kujitokeza kugombea nyadhifa za uongozi huku akisisitiza umuhimu wa mabadiliko ya kisiasa na maendeleo kote nchini.

Mama Kanisa alimwambia nini Sifuna baada ya kurushiwa vitoa machozi Kakamega?

Akizungumzia matamshi yake wakati wa mkutano wa Kakamega, alifichua kuwa mmoja wa marafiki za mamake kutoka kundi la kanisa alipiga simu na kumkosoa kwa baadhi ya maneno aliyoyasema baada ya wafuasi wake kurushiwa vitoa machozi.

“Alinipigia simu na kusema alisikitishwa sana na baadhi ya matamshi yangu huko Kakamega baada ya kurushiwa vitoa machozi. Lakini unajua, vitoa machozi vina namna ya kuchochea hisia fulani. Kwa hivyo nilimwambia kwamba mara nyingi watu hawajui lini watarushiwa vitoa machozi, na tukio likishafanyika, unaweza kupaza sauti au hata kutamka neno lisilofaa,” alisema.

Pia soma

“Cheki Mnyama”: Edwin Sifuna Azindua Lori la Kifahari Atakalotumia kwa Kampeni ya Linda Mwananchi

Wakati wa tukio hilo, Sifuna aliyekuwa thabiti alisisitiza kuwa mkutano huo usingesitishwa na akatoa maneno makali dhidi ya wanaodaiwa kuhusika na vurugu hizo.

Baadaye, umati wa watu ulitulia na kuanza kuimba nyimbo za ukombozi.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *