
Geita. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Uhusiano), Deus Sangu amezindua kampeni ya mafunzo kwa wajasiriamali wadogo ambayo ni sehemu ya programu za uhamasishaji masuala ya usalama na afya kazini kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Aprili 28, 2026 huku akisisitiza usalama kwenye uchimbaji.
Kampeni hiyo imeanza kwa kutoa mafunzo kwa Umoja wa Wanawake Wachimbaji Bukombe (Wawabu) wanaofanya shughuli za uchimbaji madini katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita ambayo yametolewa mwishoni mwa wiki.
Akifunga mafunzo ya siku moja kwa wanawake zaidi ya 350 jana Februari 23, 2026, Sangu amesisitiza juu ya umuhimu wa kuzingatia masuala ya usalama na afya katika shughuli za uchimbaji madini kwa wachimbaji wadogo, ambao mazingira yao ya kazi yana vihatarishi vingi na teknolojia duni.
“Tunafanya mafunzo haya kwa kutambua umuhimu wake kwa wachimbaji wadogo. Tumekuwa tukipata taarifa za matukio mengi ya ajali hususan kwa wachimbaji wadogo kufukiwa na vifusi wakiwa wanatekeleza majukumu yao.
“Hii ni kutokana na kuwa uchimbaji wenu mara nyingi hautumii teknolojia za kisasa ambazo ni ghali na upatikanaji wake ni mgumu,” amesema.
Ameongeza kuwa: “Nimefurahi sana kuonana na kundi la wachimbaji wanawake zaidi ya 350 kwani mara nyingi tumezoea kuona shughuli hizi zinafanywa na wanaume tu. Hivyo, ninawapongeza sana na sisi tutaendelea kuunga mkono jitihada zenu kwa kuwawezesha kufanya kazi kwa tija na katika hali ya usalama.”
Katika maagizo yake, Waziri Sangu amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha), Khadija Mwenda kuhakikisha mpango huo wa mafunzo unakuwa endelevu na kuyafikia makundi mengi zaidi ya wachimbaji wadogo na wajasiriamali katika sekta nyingine za kiuchumi.
Aidha, Waziri Sangu ametoa rai kwa wachimbaji wadogo kuzingatia masuala mbalimbali waliyofundishwa katika mafunzo hayo ikiwa ni pamoja na matumizi endelevu ya vifaa kinga ambavyo baadhi vimetolewa na Osha kupitia programu hiyo.
Akizungumza nje ya ukumbi wa mafunzo, Mtendaji Mkuu wa Osha, Khadija Mwenda amesema lengo la programu ya mafunzo kwa makundi mbalimbali ya wajasiriamali wadogo ni kuwatambua na kuwajengea uelewa wa masuala ya usalama na afya ili kuongeza kiwango cha uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya nchini.
Aidha, ameahidi kuhakikisha kwamba mpango huo wa mafunzo unakuwa endelevu kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali.
Mwenyekiti wa Wawabu, Regina Kabogo, wameishukuru Serikali kwa uwezeshaji walioupata wa mafunzo na vifaa kinga, huku wakiomba kuwafanyia upembuzi yakinifu wa hali ya upatikanaji wa dhahabu katika vitalu 13 vinavyomilikiwa na umoja huo.
“Osha wametufundisha vitu vingi sana kuhusiana na usalama na afya katika shughuli zetu za uchimbaji madini na wametupatia baadhi ya vifaa kinga vya muhimu, jambo ambalo litatuhamasisha kufanya kazi kwa bidii ili kujiongezea kipato binafsi pamoja na mapato ya Serikali,” ameeleza.
Mafunzo yanayotolewa na Osha kwa wanachama wa Wawabu yamehusisha mada mbalimbali zikiwemo dhana ya usalama na afya mahali pa kazi, vihatarishi vya usalama na afya katika sekta ya madini, Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi pamoja na misingi ya huduma ya kwanza mahali pa kazi kwa nadharia na vitendo.