Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitizia kutekelezwa sera ya msingi ya kuendeleza na kustawisha uhusiano na nchi zenye misimamo huru na za kimapinduzi katika bara la Afrika Magharibi, hususan Burkina Faso.

Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh ametoa sisitizo hilo katika mkutano na Waziri wa Nchi, Vita na Ulinzi wa Burkina Faso Brigedia Jenerali Selestin Simpore, yaliyofanyika hapa mjini Tehran, ambapo ameshukuru na kupongeza misimamo ya serikali ya Burkina Faso katika kulaani hatua ya kutapatapa ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa kutuma salamu za rambirambi na mkono wa pole kwa Waziri wa Ulinzi.

Akiashiria umuhimu na nafasi ya bara la Afrika katika sera za nje na za ulinzi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan nchi za bara hilo zenye misimamo huru, Waziri wa Ulinzi wa Iran ametilia mkazo kutekelezwa sera ya msingi ya kuendeleza na kustawisha uhusiano na nchi zenye misimamo huru na za kimapinduzi katika eneo la Afrika Magharibi, na hasa Burkina Faso.

Aidha, Jenerali Nasirzadeh ameyaelezea mapinduzi yaliyojiri kwenye eneo la Sahel katika nchi za Burkina Faso, Niger, na Mali kuwa ni harakati ya umma dhidi ya sera za kikoloni; na akazungumzia pia kuongezeka mshikamano na utangamano, pamoja na kuchukuliwa hatua inayostahiki pongezi na nchi hizo tatu ya kuunda Muungano wa Sahel wa kukabiliana na mashinikizo ya nchi za Magharibi.

Jenerali Nasirzadeh ameashiria pia kuendelea njama za nchi za Magharibi zinazolenga kudhoofisha uhuru na mamlaka ya kujitawala ya Burkina Faso, na akasisitiza uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa nchi zenye misimamo huru.

Katika mkutano huo na Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Waziri wa Nchi, Vita, na Ulinzi wa Nchi ya Burkina Faso Jenerali Celestine Simpoure, ametoa rambirambi kwa taifa la Iran na heshima kwa mashahidi wa Vita vya Siku 12, na akausifu Muqawama wa wananchi wa Iran kwa kusema: Tunaheshimu Muqawama wa watu wa Iran, ambao wametetea utambulisho na uhuru wao na kuulinda dhidi ya hatua zote za unyongeshaji za ubeberu.

Jenerali Simpore amebainisha: “Tunaamini kuwa dunia inaweza kuwa na amani kamili ikiwa uhusiano wa kibeberu kati ya nchi mbalimbali utavunjwa na kupatiwa fursa zaidi haki na amani”…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *