
Katibu Mkuu wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Ukombozi wa Palestina (PLO), Azzam al-Ahmad amesema, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS si shirika la kigaidi na ameukataa wito wa kupokonywa silaha zake huku akibainisha kuwepo mipango ya kufanya mazungumzo kuhusu uwezekano wa harakati hiyo kujumuishwa katika PLO.
Akizungumzia katika mahojiano maalumu na gazeti la Al-Shorouk la Misri, al-Ahmad amezungumzia masuala muhimu ya kisiasa yanayoukabili uongozi wa Palestina, ikiwa ni pamoja na utawala wa baadaye wa Ukanda wa Ghaza, uhusiano kati ya PLO na Hamas, na shinikizo la kimataifa la kuifanya mageuzi serikali ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina.
Afisa huyo mwandamizi wa Palestina, aliyechaguliwa katika wadhifa wake huo Mei iliyopita kufuatia kuteuliwa Hussein al-Sheikh kuwa Makamu wa Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, amesema, majadiliano yataanza hivi karibuni kuhusu uwezekano wa Hamas kuwa na uanachama katika muundo wa PLO.
Al-Ahmad amekosoa vikali mapendekezo ya Marekani yanayohusu kufanyiwa mageuzi Mamlaka ya Ndani ya Palestina, akibainisha kuwa “hayawezekani” na yana madhara kwa utambulisho wa kitaifa wa Palestina. Amesema masharti hayo yamejumuisha matakwa ya kuifanyia marekebisha mitaala ya masomo katika maskuli kwa kuondoa nembo kama vile ramani na bendera ya Palestina, matakwa ambayo ameyatupilia mbali na kusema hayakubaliki.
Akizungumzia matukio ya Oktoba 7, al-Ahmad amelielezea shambulio hilo kama “kosa la kimkakati”, na kubainisha kuwa Wapalestina wamelipa gharama kubwa kwa upande wa maafa na uharibifu.
Afisa huyo wa PLO amekosoa pia mjibizo uliotolewa na Waarabu kwa vita hivyo, akisema, mbali na Misri na Jordan, mataifa ya Kiarabu yameshindwa kwa kiasi kikubwa kuchukua hatua madhubuti ili kuzuia kuhamishwa Wapalestina katika ardhi yao…/