
Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imemtangaza Aisha Mohamed kuwa mjumbe wa bodi ya kampuni hiyo, na anatarajiwa kuchangia katika kuimarisha na kukuza zaidi shughuli za kampuni hiyo ya habari nchini.
MCL, ambayo ni kampuni tanzu ya Nation Media Group (NMG), imeeleza kuwa ujio wa Aisha unaongeza nguvu mpya katika uongozi wa kimkakati wa kampuni, hasa katika kipindi hiki ambacho sekta ya habari inapitia mabadiliko makubwa ya kiteknolojia na kibiashara.
Taarifa iliyotolewa leo, Februari 25, 2026, imemtaja Aisha kuwa mtendaji mwenye uzoefu mpana katika masuala ya uwekezaji, usimamizi wa mitaji na mageuzi ya kiutendaji.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kwa sasa Aisha anahudumu kama Ofisa Mtendaji Mkuu wa GSM Group of Companies, akisimamia mikakati, utendaji na upangaji wa rasilimali katika kampuni zinazojihusisha na usafirishaji na ugavi, viwanda, biashara, mali isiyohamishika pamoja na uwekezaji ndani na nje ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Taarifa imeendelea kufafanua kuwa, katika nyadhifa zake mbalimbali, amesimamia miradi mikubwa ya miundombinu, muunganiko na ununuzi wa kampuni, uboreshaji wa mifumo ya ukwasi, pamoja na mageuzi ya kidijitali na kiutendaji yaliyoimarisha mifumo ya utawala bora na kuongeza tija ya taasisi.
Akiwa na shahada ya kwanza ya Uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Minnesota na shahada ya uzamili ya uchambuzi wa biashara na sayansi ya uamuzi kutoka Chuo Kikuu cha Leeds Aisha anatambulika kwa umahiri wake wa masuala ya fedha na matumizi ya takwimu katika kufanya maamuzi ya kimkakati.
Uwezo huo unatarajiwa kuisaidia MCL katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali, kupanua vyanzo vya mapato ya kidijitali na kujenga mifumo endelevu ya kibiashara katika mazingira yenye ushindani mkali wa kimataifa.
Akizungumzia uteuzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya MCL, David Nchimbi, amesema kuwa ujio wa Aisha unakuja katika kipindi muhimu ambacho kampuni inaendelea kujipanga kwa ajili ya ukuaji endelevu, hususan katika mazingira ya vyombo vya habari yanayobadilika kwa kasi.
“Tunafurahi kumkaribisha Aisha Mohamed katika Bodi ya MCL. Uzoefu wake wa kimkakati katika usimamizi wa mitaji, kuimarisha utawala bora na kuongoza mabadiliko unakuja katika kipindi muhimu cha safari ya MCL.
“Tunapoiweka kampuni katika nafasi ya kufikia ukuaji endelevu katika mazingira ya vyombo vya habari yanayobadilika kwa kasi, uzoefu wake katika sekta mbalimbali na masoko ya kikanda utaimarisha maono yetu ya muda mrefu, kuongeza uwajibikaji na kuimarisha uwezo wa bodi kuiongoza MCL katika hatua inayofuata ya ubunifu na mchango chanya,” amesema.
Amesema kuwa uzoefu wake katika sekta mbalimbali na masoko ya kikanda utaimarisha maono ya muda mrefu ya kampuni, kuongezea nguvu katika uwajibikaji na kuongeza uwezo wa bodi kuiongoza kampuni katika hatua mpya ya ubunifu na mchango chanya.
Mbali na majukumu yake ya uongozi wa kibiashara, Aisha ni mtetezi wa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi, uwezeshaji wa vijana, pamoja na mawasiliano yenye tija katika biashara, maadili yanayoendana na dhamira ya MCL ya kuendeleza uandishi wa habari unaowajibika na kuchangia maendeleo ya taifa.