
Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, ametangaza fursa ya msamaha kwa wapiganaji wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) ikiwa wataweka silaha zao chini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Baraza Kuu la Utawala la Sudan, Jenerali Al-Burhan ametoa matamshi hayo katika mahafali ya kuhitimu kwa kundi jipya la maafisa katika Chuo cha Jeshi la Wanamaji huko Omdurman, magharibi mwa mji mkuu, Khartoum.
Al-Burhan amebainisha kuwa jeshi la Sudan na wananchi wataendelea kupigana hadi RSF “itakaposhindwa” na nchi “ikasafishwa” na uwepo wa kundi hilo.
“Hatuna chaguo jengine isipokuwa kuendelea na vita hadi mwisho wake, au adui ajisalimishe na kuangamizwa,” amesisitiza mkuu huyo wa Baraza la Utawala la Sudan.
Ameashiria tena fursa aliyotoa ya “msamaha kwa wapiganaji waliopotoshwa”, akiongeza kwa kusema: “Milango ya toba iko wazi, na tukiwa kama Wasudan, tunafungamana na tunu kuu zinazohitajika ili kuliunganisha taifa.”
Aidha, Jenerali al-Burhan amesema, vikosi vya ulinzi havina uadui na mrengo wowote uliobeba silaha kwa kuchochewa au kutokana na taarifa za upotoshaji. Amewataka wote hao kuweka silaha zao chini na kurudi, akiongeza kwamba, yeyote atakayechagua kusimama pamoja na nchi atapokelewa…/