IRINGA: MBUNGE wa Mufindi Kusini na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ameanza zoezi la kujenga ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo zima la Mufindi Kusini, hatua itakayosaidia kutoa huduma bora kwa wanachama na wananchi.
Akizungumza leo katika ziara yake ya mwendelezo katika jimbo lake la Mufindi Kusini, Kihenzile amesema kuwa zoezi hilo litahusisha ujenzi wa ofisi katika kata 16, na lengo ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, huku akiwataka wanachama, viongozi, wadau, na marafiki wa chama kutoa ushirikiano katika ukamilishaji wa miradi hiyo.
“Chama chetu ni kikongwe na kimeweza kutawala muda mrefu, hivyo ni lazima tukithamini. Kule ambapo kuna ofisi tutaziboresha, na kule ambapo hakuna, tumeshaanza kujipanga kwaajili ujenzi,” amesema Kihenzile.

Akisoma risala mbele ya Mbunge, Katibu wa CCM Kata ya Makungu, Yona Kyando, ameelezea changamoto zinazokabili kata hiyo, ambapo amesema baadhi ya matawi yana ofisi zilizochakaa ambazo zinahitaji kuvunjwa na kujengwa upya, na hivyo Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya kata imekubaliana kutafuta wadau na wapenzi wa chama ili kuanza mchakato wa ujenzi wa ofisi za matawi.
Kyando pia amemuomba Mbunge Kihenzile kuwaunga mkono katika kufanikisha zoezi hilo ili kila kata iwe na ofisi yake ya chama.