Dar es Salaam. Msimu wa 26 wa mashindano ya mabara ya kuhifadhi Quran tukufu yanatarajiwa utafanyika Machi Mosi, 2026 katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Al-Hikma Foundation, ambao ni waandaaji wa mashindano hayo, Sheikh Nurdin Kishki amewaambia wanahabari leo Jumatano Februari 25,2026 washiriki 18 wa mchakato huo wataanza kuwasili kesho Alhamisi Februari 26,2026.
Sheikh Kishki amesema kutoka Bara la Amerika Kaskazini wanatoka washiriki wawili na Amerika Kusini watatoka wawili pia. Wakati katika Bara la Ulaya watatoa washiriki watatu.
“Bara la Australia kutakuwa na washiriki wawili, vivyo hivyo katika bara la Asia kutakuwa na washiriki wawili pia. Katika Bara la Afrika, kutakuwa na washiriki kutoka nchi za Zambia, Uganda, Kenya na kisiwa cha Reunion,” amesema.
Kwa upande wa Tanzania, Sheikh Kishki amesema kutakuwa na washiriki watatu wakiwemo kutoka Zanzibar, huku taasisi ya Al-Hikma itatoa mshiriki mmoja.
“Jumla washiriki wa mwaka huu ni 18, tumepunguza idadi kutoka 24 ya msimu uliopita ili kuendana na muda na kuhakikisha mashindano yanaanza mapema na kumaliza mapema,” ameeleza.
Kwa mujibu wa Sheikh Kishki, mashindano hayo yatakuwa na mshindi namba moja hadi tano, akisema atakayeshika nafasi ya kwanza atajinyakulia Sh31.2 milioni.
Mwenyekiti wa Mashindano ya Mabara Kuhifadhi Quran, Sheikh Nurdin Kishik akizungumza na wanahabari.Picha na Michael Matemanga
Sheikh amesema mshindi wa pili atapata Sh20.8 milioni, mshindi wa tatu atapata Sh13 mshindi wa nne atapata Sh10.4 milioni huku mshindi wa tano atajinyakulia zawadi ya Sh7.8 milioni.
Mbali na hilo, Sheikh Kishki amesema kutakuwa na zawadi ya sauti bora ambapo mshindi atajinyakulia Sh1.3 milioni huku mshiriki mdogo kuliko wote atapata Sh1.3 milioni.
Kishki ambaye ni Mwenyekiti wa mashindano hayo amesema washiriki wote watapatiwa Sh500,000 kama kifuta jasho cha mashindano hayo ambayo mwaka huu yataanza kuanzia saa 12:15 asubuhi.
Mashindano hayo yatahudhuriwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, huku Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akitarajiwa kuwa mgeni maalumu.
Katika hatua nyingine, Sheikh Kishki amesema kutakuwa na mabadiliko kidogo katika mashindano ya mwaka huu, akisema majaji wanatoa alama huku majumuisho yakifanywa kwa njia ya kidijitali zaidi.
Mafundisho ya Quraan Tukufu yametajwa kuzalisha vijana wenye heshima na matokeo yake kuwa na Taifa lenye watu wenye maadili.
Februari 23, 2025 akitoa hotuba yake katika mashindano ya dunia ya kuhifadhi Quran, aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema Serikali inatarajia kuona elimu ya dini ikianza kutolewa mapema kwa watoto wadogo ili kuwapa misingi bora ya maadili.