Rukwa. Jamii imetakiwa kuimarisha na kuenzi utamaduni wa ushirikiano kupitia majadiliano ya mara kwa mara, hatua itakayochangia kujenga Taifa lenye ustawi na maendeleo endelevu.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kwela, wakati wa ziara yake katika Kata za Laela na Kasanzama, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, Februari 24, 2026. Ziara hiyo imelenga kuhamasisha ushirikiano, mshikamano na kuimarisha mahusiano ndani ya jamii.
Katika ziara hiyo, Waziri Sangu amesema kuwa jamii inapokuwa na mahusiano mema, utekelezaji wa majukumu ya kila mwananchi hufanyika kwa amani na utulivu, hali inayochochea ukuaji wa uchumi na ujenzi wa Taifa.
Akiwa katika mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo mkubwa wa kilovoti 400 (400kV) wa gridi ya Taifa unaotekelezwa kutoka Tunduma hadi Sumbawanga, Waziri Sangu ameielekeza kampuni ya Sinohydro Corporation Limited kuhakikisha kazi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa umakini, ili wananchi wa Sumbawanga waweze kupata umeme wa uhakika.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Waziri huyo amesema Serikali imedhamiria kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inakamilika kwa wakati ili wananchi wanufaike nayo na kuboresha maisha yao.
Waziri Deus Sangu wakati akizungumza na walimu katika shule ya sekondari Uchile
Katika hatua nyingine, Waziri Sangu amesema ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo pamoja na mifumo ya usimamizi wa rasilimali watu, huku akipongeza juhudi za mkandarasi, Sinohydro, katika kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa viwango vinavyokidhi matakwa ya kisheria na kitaaluma.
Aidha, amemuelekeza mkandarasi huyo kuzingatia kwa makini masuala ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi, pamoja na kuendelea kuchangia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa mujibu wa sheria.
Akitoa wasilisho mbele ya Waziri, mwakilishi wa kampuni ya Sinohydro ambaye pia ni Meneja wa Rasilimali Watu na Mahusiano, Maghembe Noni ameahidi kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali na kuzingatia sheria na taratibu zote za kazi katika utekelezaji wa mradi huo.
Baada ya kukagua miradi mbalimbali katika halmashauri hiyo, Waziri Sangu alikutana na viongozi wa dini, taasisi na mashirika binafsi. Katika kikao hicho, amewataka madiwani, maafisa tarafa na watendaji wa kata kufanya kazi kwa ushirikiano bila kujali dini, chama au kabila, akisisitiza kuwa lengo kuu ni kusimamia miradi ya maendeleo na kuchochea ukuaji wa uchumi kwa kubuni na kutekeleza miradi yenye tija.
Katika kongamano la wadau wa mahusiano lililofanyika, wananchi walipata fursa ya kuwasilisha kero zao.
Waziri Sangu amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kuleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali.
Amesema miongoni mwa kero zilizotajwa ni pamoja na miundombinu ya barabara, na kwamba kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Serikali ina mpango wa kujenga barabara ya Kanondo–Muze, ambayo itafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa, hususan kutokana na mkoa huo kuwa mzalishaji mkubwa wa zao la mpunga.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi akiwemo Grory Mathew, wamesema ili kuimarisha mahusiano mema, viongozi wanapaswa kuwashirikisha wananchi katika miradi ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za mapato na matumizi.
“Tunaposhirikishwa na kupewa taarifa mbalimbali, ikiwemo kusomewa mapato na matumizi, inatusaidia kuelewa na kutumia vyema fursa zinazopatikana katika maeneo yetu,” amesema Grory.
Waziri Sangu yupo katika ziara ya kikazi katika Jimbo la Kwela, ambapo pia alikagua miradi ya maendeleo ikiwemo Shule ya Sekondari ya Wasichana Rukwa iliyopo Kata ya Laela na Shule ya Sekondari Uchile iliyopo Kata ya Kasanzama.