Dar es Salaam. Hakuna safari nyepesi katika maisha, kama anavyosimulia Miss Tanzania 2022, Halima Kopwe alipozungumza na Mwananchi kuhusu safari yake ya urembo, changamoto alizopitia na dhamira yake ya kuendelea kuhamasisha wanawake kutokana na miradi yake ya kijamii.
Halima anasema taji halikuwa mwisho wa ndoto zake, bali mwanzo wa jukumu kubwa la kuwakilisha wanawake wanaotamani mafanikio na mabadiliko.
ALIPOTOKEA
Halima alikulia mkoani Mtwara katika familia yenye misingi ya maadili, nidhamu na bidii. Kabla ya kuingia katika shindano la Miss Tanzania, alikuwa anatafuta mwelekeo wake na jukwaa linaloweza kufanikisha ndoto zake.
“Nilikuwa msichana wa kawaida kabisa. Lakini mwenye ndoto zisizo za kawaida, nilijua lazima nitafute njia ya kugusa maisha ya watu wengi zaidi.”
“Safari yangu ya kuelekea kwenye kulipata taji haikuwa rahisi, ilikuwa na presha ya mashindano, matarajio ya jamii na sauti za wakosoaji waliodhani urembo hauwezi kwenda sambamba na ajenda za kijamii. Hata hivyo changamoto hizo zilinijenga na kunifanya niwe imara zaidi na kuna wakati unajiuliza kama kweli utaweza, lakini nilijifunza kujiamini zaidi,” anasema.
Katika shindano la Miss Tanzania 2022, Halima alishinda zawadi ya gari aina ya Mercedes Benz lenye thamani ya Sh40 milioni na pesa taslimu Sh10 milioni na uwakilishi wa Shindano la Urembo la Dunia (Miss World 2022) lililofanyika mwaka 2024 huko India na kung’ara.
Halima alikuwa ni mrembo wa nne tangu shindano hilo kuanza kuratibiwa na Kampuni ya ‘The Look’ mwaka 2018 akitanguliwa na Queen Elizabeth Mukune, Sylvia Sebastian na Rosemary Manfere.
JUKUMU LILIMTESA
Halima anasema hakuna kipindi alikaribia kukata tamaa kama kipindi anatumikia nafasi ya Miss Tanzania kutokana na kuelemewa na majukumu mazito ya uwakilishi.
“Ilifikia hatua nilikabiliwa na uchovu wa maandalizi na mzigo wa kuwakilisha taifa. Lakini kila ninapokumbuka dhamira yangu ya kusaidia jamii kutokana na kampeni za damu, niliona sababu ya kuendelea na sababu yangu ilikuwa kubwa kuliko hofu yangu,” anasema kimwana huyo.
Halima aliyeingia katika 10 Bora katika Miss World 2022 lililofanyika India katika kipengele cha ‘Beauty with Purpose Project’ kutokana na kampeni yake ya ‘Damu Yangu Kizazi Changu’ uliolenga kuboresha afya kwa Wanawake wajawazito na watoto nchini kupunguza vifo kwa wahusika hao.
KILICHOMSUKUMA MISS TZ
Halima alipoulizwa kitu gani kilichomsukuma hata akaingia katika shindano la urembo la Miss Tanzania, alisema:
“Unajua Miss Tanzania ilikuwa zaidi ya shindano la urembo, ilikuwa jukwaa la sauti, sasa nikaona kutokana na nafasi hiyo, naweza kuanzisha na kuendeleza mradi wangu wa My Blood Generation, unaohamasisha uchangiaji wa damu salama ili kupunguza vifo vya mama na mtoto”.
Anasema hata hivyo, kama watu wengine alikumbana na changamoto katika safari yake ya kutimiza ndoto za kusaidia jamii.
“Baada ya taji, majukumu yangu yaliongezeka, safari za kuhamasisha jamii, kushirikiana na taasisi za afya na kuzungumza na vijana zimekuwa sehemu ya maisha yangu ya kila siku,” anasema Halima na kufafanua;
“Changamoto kubwa ilikuwa ni kubadilisha mtazamo wa watu kuhusu kuchangia damu, lakini naamini elimu ndiyo suluhisho na naona kizazi kipya kina nafasi ya kuleta mabadiliko makubwa ikiwa kitashirikiana.”
Anasema anachoshukuru ni kujituma kwake na kutimiza ndoto zake zilizaa matunda na kumpaa mafanikio anayojivunia.
“Mafanikio yameongeza uwajibikaji wangu binafsi na kijamii, naona sasa kila hatua anayopiga inaangaliwa na wasichana wengi kwa kuniona mimi ni kama mfano wa kuigwa,” anasema Halima na kuongeza;
“Taji limeongeza wajibu wangu, najua kuna wasichana wengi wananiangalia kama mfano, kutokana na kampeni zangu nimeweza kuhamasisha vijana kushiriki katika uchangiaji damu na kujitolea kwa jamii.”
Juu ya kitu kilichompa msukumo wa kuisaidia jamii katika ishu ya uchangiaji damu, Halima anajibu kwa kusema;
“Msukumo wangu unatokana na kuona athari chanya ninazoziona katika maisha ya wengine, kujua damu inaweza kuokoa maisha ya mama au mtoto, inanipa nguvu ya kuendelea kila siku.
“Natamani kupanua wigo wa mradi wangu wa afya uwe wa kitaifa zaidi, huku nikiendelea kushirikiana na wadau wa afya ili kuhakikisha damu salama inapatikana kwa wote wanaohitaji.”
UJUMBE KWA WANAWAKE
“Mimi naamini wanawake wanapaswa kuendelea kupigania elimu, afya na usawa wa fursa, kwa mwanamke anayekutana na vikwazo kila siku, ujumbe wake ni wa matumaini na uthubutu,” anasema Halima na kufafanua;
“Wanawake wakiamua kusimama pamoja, hakuna kinachoweza kuwazuia kitu kikubwa ni usikate tamaa, watambue kila changamoto ni sehemu ya safari, simama tena, hata kama umeanguka mara ngapi.
Pia siku ya Wanawake Duniani si maadhimisho tu, ni ukumbusho mwanamke akiamua kuinuka, anaweza kubadilisha si maisha yake peke yake, bali kizazi kizima.”