Dar es Salaam. Mwanamitindo maarufu nchini, Jasinta Makwabe, amewataka wanawake kujitambua, huku akiwapa somo la namna ya kuikuza thamani yao.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu safari yake ya mafanikio, amesisitiza mwanamke anapaswa kuwa na viwango katika maisha yake.
“Lazima kwanza ujitambue wewe ni nani, unataka kufanya nini na unataka kufika wapi. Ukishajitambua unaweka standadi yako kwamba mimi nafanya hiki na hiki, lakini hiki sifanyi. Sio lazima ufanye kila kitu hapana.
“Ukishajua unapenda kitu fulani, weka nguvu yako na akili kwenye hicho kitu, ili kikufikishe sehemu fulani, uwe na msimamo sio unafanya na kuacha. Pia mwanamke lazima ujiheshimu, ukijiheshimu watu watakuheshimu, ukijichukulia poa kila mtu atakuchukulia poa watakutumia na kukuacha,”amesema Jasinta
Amesisitiza ni muhimu kuwa na njia mbalimbali za kujipatia kipato hata kama umeajiriwa.
“Hatakama unafanya kazi hakikisha unabiashara nyingine ambayo inakuingizia pesa. Kwasababu ukiwa na pesa yako hakuna mwanaume atakutumia hovyo, au kukudharau kwani utaweza kujihudumia mwenyewe, kujilipia kodi, ukasafiri na kuhudumia familia yako,” amesisitiza.
Mwanamitindo huyo ambaye pia amekuwa akigusa maisha wengine kwa kuwasaidia wenye uhitaji. Amesema mwanamke ananafasi ya kusaidia jamii.
“Kitu cha kusaidia watu ni kutoka ndani ya moyo wa mtu. Mimi ni mtu ambaye sipendi kuona mtu anateseka. Nikiwa na uwezo wa kusaidia yaani sijali iwe nakujua iwe sikujui.
“Kumsaidia mtu sio lazima uwe bilionea. Nafurahia nikiona sasahivi mastaa wengi Bongo wakitoa misaada napenda sana kama ningekuwa bilionea ningesaidia dunia nzima. Lakini ndio huwezi kumsaidia kila mtu. Ukiweza kumsaidia hata mmoja unabarikiwa sana na huwezi kupungukiwa kamwe,” amesema.