MWANZA; MKAZI wa Mtaa wa National uliopo Ngudu, wilayani Kwimba mkoani Mwanza, Joyce Emmanuel, amesema kukamilika kwa jengo la watoto njiti kwenye Hospitali ya kwimba ni ukombozi kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Akizungumza nyumbani kwake wakati wa ziara ya viongozi mbalimbali, Joyce amesema alijifungua mapacha akiwa na ujauzito wa miezi sita, kila mmoja akiwa na uzito wa kilo 1.3. Hata hivyo, kutokana na ukosefu wa vifaa vya kuhudumia watoto njiti katika zahanati ya eneo lao, walilazimika kusafiri umbali mrefu kwenda Hospitali ya Bugando Mwanza, hali iliyosababisha mtoto mmoja kupoteza maisha njiani.

Amesema hayo alipotembelewa na Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania, Dk Alex Gasasira, aliyeambatana na viongozi wa taasisi ya Doris Mollel Foundation (DMF), Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ng’wilabuzu Ludigija, pamoja na viongozi wengine.

“Mimi ni mama wa watoto sita,  nikiwa na ujauzito wa pacha wa miezi sita. Waliniambia watoto wamekaa tofauti tumboni, mmoja kichwa chini na mwingine miguu juu. Nilijifungua Kulwa na Doto. Kulwa alikuwa vizuri, lakini Doto alikuwa na hali mbaya sana,” amesema Joyce.

Amesema kutokana na kukosa huduma za watoto njiti katika kituo cha afya cha karibu, walishauriwa kwenda Hospitali ya Bugando, lakini walipokuwa njiani mtoto mmoja alizidiwa na kupoteza maisha.

Anasema mtoto aliyesalia alipofikishwa Bugando alipimwa na baadaye kuendelea kuimarika kiafya hadi kufikisha uzito wa kilo 1.5 na kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Kwa sasa mtoto huyo ana umri wa miaka miwili na miezi kadhaa, lakini Joyce amesema gharama kubwa za matibabu zimemwacha katika hali ngumu ya maisha.

Ameishukuru DMF  chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake Doris Mollel kwa kukamilisha ujenzi wa jengo la kisasa lenye viwango vya kimataifa kwa ajili ya kuhudumia watoto njiti katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, akisema litapunguza vifo vinavyotokana na kuchelewa kupata huduma.

“Huduma zikisogezwa karibu, gharama zitapungua na maisha ya watoto yataokolewa. Tunashukuru sana kwa hospitali hii,” amesema.

Kwa upande wake, Dk Gasasira ameipongeza DMF kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, akisema mradi huo utaokoa maisha ya watoto wengi wanaozaliwa kabla ya wakati.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ng’wilabuzu Ludigija, amesema ujenzi wa jengo hilo ni hatua muhimu katika kupunguza vifo vya watoto njiti ndani ya wilaya hiyo na halmashauri jirani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *