Katika kujibu hatua haramu ya Umoja wa Ulaya dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeyataja majeshi ya majini na anga ya nchi zote wanachama wa umoja huo kuwa mashirika ya kigaidi.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza katika taarifa ya kujibu hatua hiyo iliyo kinyume cha sheria ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, tarehe 19 Februari 2026 kwa kusema: ‘Nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimelitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ambalo linahesabiwa kuwa moja ya vikosi rasmi vya jeshi la nchi hii, kuwa shirika la kigaidi, kinyume kabisa na misingi na kanuni za Hati ya Umoja wa Mataifa pamoja na sheria za kimataifa.’

Taarifa hiyo, imeendelea kusema, serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua hatua ya kujibu kwa kuchukua hatua sawa na ile iliyochukuliwa dhidi yake na kwa mujibu wa Ibara ya 7 ya Sheria ya “Hatua Sawa iliyochukuliwa na Marekani dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kulituhumu kuwa shirika la kigaidi ” mwaka 2018.

Imeelezwa katika taarifa hiyo kuwa, nchi zote zitakazofuata au kuunga mkono uamuzi wa Marekani wa kulitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa shirika la kigaidi zitachukuliwa hatua sawa na hizo.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran, imeeleza kuwa jeshi la wanamaji na anga la nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya litawekwa chini ya sheria hiyo na vifungu vyake ikiwemo Ibara ya 4. Hivyo, serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatambua na kuyatangaza kuwa mashirika ya kigaidi katika fremu ya sheria hiyo ya kuchukuliwa hatua sawa za kulipiza kisasi katika kukabiliana na pande hasimu.

Uamuzi wa nchi wanachama za Umoja wa Ulaya wa kulitangaza Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni la kigaidi ni ukiukaji wa wazi wa kanuni za kimsingi za Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa. Kulingana na vifungu vya hati hiyo, serikali zinalazimika kuheshimu mamlaka ya kitaifa na umoja wa ardhi wa nchi wanachama na kuepuka uingiliaji wowote katika muundo wa ndani wa nchi hizo.

Jibu la Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Kutuhumu sehemu ya vikosi rasmi vya jeshi la nchi huru kuwa gaidi kuna maana ya kuhoji mamlaka ya kijeshi na usalama ya nchi hiyo, kitendo kinachochukuliwa kuwa kinyume cha sheria za kimataifa.

Ikiegemea kanuni ya kuchukuliwa hatua sawa na Kifungu cha 7 cha sheria iliyoidhinishwa mwaka 2018, Iran inachukulia hatua yake dhidi ya Umoja wa Ulaya kama jibu la kisheria la kulipiza kisasi. Kwa mujibu wa sheria hii, nchi au taasisi yoyote inayounga mkono uamuzi wa Marekani wa kulituhumu jeshi la IRGC kuwa la kigaidi itakabiliwa na hatua sawa na hiyo.

Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni moja ya nguzo za jeshi rasmi la nchi hii. Kwa hivyo, uingiliaji wowote au mashinikizo dhidi yake huzingatiwa kama kulengwa moja kwa moja muundo wa ulinzi wa kitaifa.

Hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kulitangaza jeshi la wanamaji na anga la nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuwa magaidi inachukuliwa kuwa jibu la kistratijia na la pande kadhaa katika kukabiliana na uadui na uingiliaji wa nchi za Magharibi dhidi ya moja ya nguzo za msingi za mfumo wa ulinzi wa Iran.

Katika mtazamo wa kisiasa, uamuzi huu ni ishara ya kujitawala na nguvu katika siasa za kigeni za Iran, nchi ambayo haiko tayari kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya nchi za Magharibi. Kutangazwa taasisi za kijeshi za Ulaya kuwa za kigaidi, kivitendo, kunaweza kubadilisha milinganyo ya kisiasa kutoka kuwa ya upande mmoja na kuifanya Ulaya kuelewa kwamba hatua zao hazitapita bila kujibiwa.

Uamuzi huu pia unaimarisha mshikamano wa ndani na uungaji mkono wa wananchi kwa vikosi vya jeshi la taifa, kwa sababu jamii inaviona kama nembo ya “kutetea heshima na umoja wa ardhi ya nchi”.

Hatua ya Iran ya kuyatambua majeshi ya Ulaya kama mashirika ya kigaidi ni mstari mwekundu wa kiusalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo inachukulia tishio dhidi ya jeshi la Iran kuwa tishio kwa uwepo na mamlaka yake ya kitaifa. Katika ngazi ya mikakati jumla, hatua hii inaonya kwamba Iran itatumia zana zake zote za kisheria na kisiasa katika kujibu uingiliaji wowote wa masuala ya ulinzi na usalama wake wa kitaifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *