
JAMHURI Kihwelo ‘Julio’ baada ya kuiongoza Mashujaa katika mechi mbili akiwa kocha mkuu akishinda zote ikiwamo dhidi ya Mtibwa Sugar Ligi Kuu na ile ya Kombe la Shirikisho mbele ya Nkim, ameshtuka kisha kuomba mechi za kirafiki, huku akitoa sababu.
Kocha huyo aliyechukua mikoba ya Salum Mayanga hivi karibuni, ameliambia Mwanaspoti kuwa, ameichungulia ratiba ya mashindano zilivyo na kubaini timu hiyo ikataa bila kucheza kwa muda mrefu na hilo linaweza kuitibulia ndio maana ameamua kusaka mechi za kirafiki kujiweka sawa.
Kwa mujibu wa ratiba, Mashujaa ambayo ilishuka dimbani mara ya mwisho wiki iliyopita katika mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Nkim FC itasubiri hadi Machi 15 ili kurudi uwanjani na hicho ndicho Julio alichostukia kwamba timu inaweza kupungua kasi iwapo haitapata mechi za kirafiki kujiweka fiti.
Julio alisema kutokana na kukosa mechi za ushindani, hivi karibuni aliuomba uongozi kumtafutia mechi za kirafiki ili wachezaji waendane na maandalizi wanayoendelea kufanya.
“Mara baada ya kucheza mechi yetu ya Kombe la Shirikisho timu imeendelea na mazoezi kujiweka tayari na mechi zinazofuata ambapo Machi 15 tutacheza na Pamba Jiji kutokana na ratiba yetu kuwa mbali zaidi nimehitaji mechi za kirafiki ili kufanya mazoezi kwa vitendo,” alisema.
“Raha ya mazoezi ni kufanya na vitendo. Hatuwezi kufanya mazoezi kwa mwezi mzima bila mechi kutokana na ratiba kutokuwa rafiki kwa kukosa mechi ya mashindano, basi naamini tukipata mchezo wa kirafiki utasaidia kutambua ubora na upungufu wa wachezaji kabla ya mechi ya mashindano.”
Ofisa Habari wa Mashujaa, Steven Ndorobo alisema wameiandikia barua Bodi ya Ligi (TPLB) ili kucheza mechi za viporo dhidi ya Azam FC na Fountain Gate na kwamba wanasubiri majibu kama hilo litafanikiwa, kwani watakuwa na wakati wa kucheza mechi kabla ya Machi 15.
“Kukaa bila kucheza mwezi mzima sio afya kwa wachezaji tuliandika barua bodi ya Ligi ili tucheze mechi dhidi ya Azam FC Machi 2, lakini watakuwa na mechi dhidi ya Pamba hivyo imekuwa ngumu lakini juu ya kucheza na Fountain Gate bado tunasubiri majibu.”
Hata hivyo, kwa mujibu wa ratiba ya hatua ya 32 Bora ya Kombe la Shirikisho, Mashujaa itakuwa dhidi ya KenGold kati ya Machi 6-8, mwaka huu.