Dar es Salaam. Kabla ya kukata tamaa ukiwasikiliza mastaa hawa katika simulizi za kawaida za maisha watakupa moyo wa kuzipigania ndoto zako bila kujali upo katika mazingira gani.

Watakupa moyo kutokana na maneno na kauli zao ili kupambania kile unachoamini unataka kifanikishe maisha yako.

Katika hilo, kumbuka wapo baadhi ya mastaa ambao historia zao zilibeba ndoto, hivyo ukiwasikiliza wanaweza kukusogeza katika safari ya mafanikio.

Mwanachi linakusogezea baadhi ya mastaa ambao wana stori zinazoweza kukupa moyo wa kuendelea kupambania.

Ney wa Mitego

Msanii wa Bongo Fleva, Emmanuel Elibariki Munisi ‘Ney wa Mitego’, ingawa alianza kuimba tangu akiwa shule ya msingi (darasa la tatu), maisha yalimfanya afanye kazi ya kinyozi.

Katika mahojiano aliyowahi kufanya alisema: “Mama alinifukuza baada ya kumaliza darasa la saba. Hakupenda nifanye muziki. Nilimwambia naondoka, nitarudi kukusaidia nikiwa nimefanikiwa.”

Anaongeza: “Matokeo ya darasa la saba yalipotoka nilifaulu, lakini baada ya kuondoka nyumbani alikuwepo kaka yangu wa kitaa. Ambaye ni marehemu kwa sasa, alikuwa anaitwa James Mbawala, huyo alikuwa na saluni. Aliniambia akimaliza kazi yake ya kunyoa niwe nafagia na kulala hapo.

“Pia alisema natakiwa kujifunza kunyoa ili nisiwe naomba pesa ndogo. Nikajifunza na ilinisaidia kujilipia ada kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Pamoja na hilo, nilikaza buti kuzipambania ndoto zangu na kwa mara ya kwanza niliingia studio mwaka 1998. Hivyo Ney wa Mitego wa sasa hajaibuka ghafla, bali nilipambana.”

Bidii na kutokukata tamaa katika maisha ya msanii wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’, ndivyo vilivyompa heshima katika tasnia hiyo. Mbali na muziki, alikuwa anapenda kucheza mpira wa miguu na kufanya biashara ndogo ndogo.

Katika wimbo wake Never Give Up, anaelezea maisha yake kabla ya kupata mafanikio na umaarufu, akisema kuna wakati alikuwa hajui alale wapi, kula kulikuwa siyo kwa uhakika, na alifanya biashara mbalimbali.

Msanii anayetamba kwenye muziki wa Bongo Fleva, Omary Ally Mwanga maarufu Marioo alikuwa mfanyakazi wa gereji kabla ya kutoboa kimuziki na kilichombeba ni hakukubali kudidimiza ndoto zake licha ya mazingira magumu kumzunguka.

Marioo anayetamba na nyimbo mbalimbali kama ‘Hakuna Matata’, ‘Mi Amor’, ‘For You’ na ‘Asante’, aliwahi kufanya mahojiano na kuelezea namna alivyosota gereji hadi kutoboa kimaisha.

“Nilianza kujifunza kutengeneza tenki za mafuta, kuchomelea bati. Nilifanya vizuri kwa sababu nilijua suala la kusoma limeshindikana. Hivyo nikaamua kukaza buti katika kazi hiyo. Gereji nimefanya miaka mitatu, baadaye nikaanza kuzipambania ndoto zangu za muziki,” anasema.

Jay Melody

Mmoja wa mastaa wenye sauti nyororo katika muziki wa Bongo Fleva, Jay Melody, kabla hajatoboa kimuziki na kuwa staa, aliwahi kuuza mitumba na kufanya kazi ya useremala na alikuwa analipwa Sh15,000 kwa wiki, akaona hawezi kutoboa.

“Katika kuuza mitumba nilikuwa nafanya kazi ya kuita wateja. Unaenda na gari lenye nguo, halafu mnashuka mnapotea; baadaye mnajifanya mnarudi kununua ili kuvutia watu. Baadaye nikaanza kufanya muziki na sasa ndiye Jay Melody mnayemwona leo,” anasema.

Msanii wa Bongo Fleva, Sunday Mangu ‘Linex Sunday Mjeda’, kabla ya kuwa msanii mkubwa aliwahi kupitia mafunzo ya jeshi, lakini akaamua kuweka nguvu yake katika kipaji chake.

“Nilikuwa napenda kujifungia ndani na kuimba mwenyewe, ndipo mjomba wangu aliniambia nina uwezo mkubwa wa kuimba. Hapo ndipo safari ya kwenda studio ikaanza. Ndiyo maana sibabaishwi na ustaa; niliujenga tangu mwanzo,” anasema Linex.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *