
Dar es Salaam. Makamu wa Rais wa zamani, Chuo Kikuu cha Minnesota, aliyeshughulika na utafiti, Brian Herman, katika mahojiano aliyoyafanya baada ya kashfa ya fedha za Epstein vyuoni alisema, “kuna wito mkubwa na muhimu wa kupata fedha kwa ajili ya kuwezesha kazi za kitivo na wafanyakazi.
“Presha siku zote imekuwepo, lakini bado unaweza kutafuta fedha kwa njia zenye maadili na uadilifu unaokubalika.”
Marekani, asilimia 53 mpaka 55 ya fedha ya kuwezesha utafiti hutolewa na Serikali kuu, kama vile Taasisi ya Taifa ya Afya (NIH) na Mfuko wa Taifa wa Sayansi (NSF).
Asilimia nane hutoka taasisi binafsi na asasi zisizo za kiserikali zisizolenga faida, mfano, Jumuiya ya Saratani Marekani (ACS).
Hesabu hiyo huacha mzigo mkubwa kwa menejimenti za vyuo kutafuta fedha ili kufanikisha malengo. Na hapo ndipo watu kama Epstein hufikiwa. Vyuo hupokea fedha bila kujiridhisha zilipotoka na usafi wa mtoaji.
Mjadala kuhusu fedha za Epstein zilivyotia najisi vyuo vikuu ni mrefu. Ni kipimo kuwa athari zilizoachwa na mhalifu huyo wa makosa ya kingono kwa mabinti wadogo, zimeenea na kugusa maeneo mengi.
Wakati huohuo, wazito wa dunia (world’s behemoths), wanapitishwa kwenye ulimwengu ambao haikudhaniwa kama wangewahi kupita.
Uliwahi kuwaza mwanamfalme Andrew Mountbatten-Windsor, mtoto wa Malkia Elizabeth na mdogo wa Mfalme Charles III wa UK, angekamatwa na kuwekwa mahabusu? Februari 19, 2026, ikiwa ni siku ya Andrew kusherehekea kutimiza miaka 66 ya kuzaliwa kwake, alijikuta anaadhimisha akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Polisi wa Kituo cha Norfolk, Uingereza, walimkamata Andrew kwenye kasri lake la kifalme, Royal Lodge na kwenda naye kituoni.
Wakati Andrew akiwa kituo cha polisi, uchunguzi ulifanyika ndani ya Royal Lodge ili kubaini chochote ambacho kinatosha kumfungulia mashitaka mwanamfalme huyo.
Alhamisi usiku (Februari 19), polisi walimwachia Andrew kwa dhamana ya kiuchunguzi.
Taarifa ya polisi ilieleza kwamba, uchunguzi unaendelea dhidi ya Andrew, kubaini kama kuna makosa yoyote aliyafanya, hasa kutoa siri za Serikali kwa Epstein.
Kwa miaka 10, Andrew alikuwa mshauri wa biashara wa Serikali ya UK. Nyaraka za Mafaili ya Epstein, zimeonesha kuwa, Epstein na Andrew walikuwa wakijadiliana kuhusu kunufaika kupitia cheo cha Andrew.
Polisi wanachunguza kama aliitumia vibaya ofisi ya umma na ikiwa alivujisha siri za ofisi kwa Epstein. Wananchi UK, wao wanataka Andrew afikishwe mahakamani kwa makosa ya kusafirisha watu kwa ajili ya ngono, pia kuwafanyia mabinti wadogo ukatili wa kingono.
Mafaili ya Epstein yamemtaja Andrew, mwathirika wa uhalifu wa Epstein, Virginia Giuffre, ameshuhudia na kitabu ameandika akimtaja waziwazi kuwa alimbaka alipokuwa na umri wa miaka 17.
Pamoja na kwamba kuna watu wanaona haijatosha kwa Andrew, lakini ukweli ni kuwa tukio la kukamatwa kwake, akiwa mtoto wa familia ya kifalme, ni la kipekee ndani ya miaka 380 iliyopita.
Kabla ya Andrew, mtu wa mwisho kukamatwa na kufikishwa polisi kutoka ndani ya familia ya kifalme UK, alikuwa Mfalme Charles I, ambaye alishitakiwa kwa uhalifu, kisha akanyongwa.
Hiyo ilikuwa karne ya 17, wakati wa vita ya kiraia ya Uingereza. Mfalme Charles I liposhindwa vita, zahama ikamkuta.
Waziri Mkuu wa zamani wa Norway, Thorbjorn Jagland, tangu Mafaili ya Epstein yalipowekwa wazi Januari 30, 2026, amekuwa kwenye hekaheka na polisi, ambao tayari wameshamfungulia mashitaka ya rushwa.
Polisi Norway pia wanachunguza kama kuna makosa mengine Jagland aliyafanya kwa kushirikiana na Epstein. Kipindi uchunguzi ukiendelea na kesi ya rushwa ikiwa imeshafunguliwa, tayari Jagland alishakamatwa mara moja na kuhojiwa zaidi kuhusu uhusiano wake na Epstein.
Jagland amefunguliwa mashitaka, baada ya Baraza la Umoja wa Ulaya (CoE), kumwondolea kinga ya kutoshitakiwa, kutokana na hadhi yake ya kidiplomasia alipokuwa Katibu Mkuu wa baraza hilo.
Kikosi cha kukabiliana na uhalifu cha Okokrim, kimekuwa kikifanya uchunguzi kwenye mali za Jagland, kuona alizipataje na kubaini ushiriki wa Epstein.
Jagland anatuhumiwa kumsaidia Epstein kupata mkopo mkubwa benki nchini Norway na DOJ wameonesha mawasiliano ya karibu baina ya wawili hao.
Sultan Ahmed bin Sulayem amepoteza kazi DP World. Sultan Ahmed ni memba wa koo ya Sulayem ambayo ina ukaribu na familia ya Maktoum, inayotawala Dubai.
Sultan huyo amekuwa mwenye ushawishi mkubwa duniani na anasifika kwa kuifanya DP World kuwa kampuni inayoaminika kwa uendeshaji wa bandari ulimwenguni.
DP World wamekuwa waendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, Tanzania, tangu mwaka 2023.
Februari 13, 2026, Ofisi ya Habari ya Serikali ya Dubai, ilitangaza uteuzi wa Abdulla bin Damithan kuwa mwenyekiti mtendaji mpya wa DP World, nafasi ambayo ilikuwa ikishikiliwa na Sultan Ahmed.
Taarifa hiyo haikutaja kabisa jina la ‘Ahmed bin Sulayem.’ Hata hivyo, dunia inatambua kuwa Sultan Ahmed ni miongoni mwa watu waliochomoza mara nyingi kwenye Mafaili ya Epstein. Jina la Sultan Ahmed limeonekana mara 322, katika nyaraka zilizowekwa wazi na DOJ hadi sasa.
Aliyekuwa Balozi wa Norway kwenye nchi za Jordan na Iraq, Mona Juul, Februari 15, 2026, alitangaza kujiuzulu wadhifa wake, baada ya kwanza kusimamishwa kazi kutokana na kashfa ya kuwahi kujenga ukaribu na Epstein. Mona pia anachunguzwa kwa makosa ya rushwa. Vyombo vya habari Norway, viliripoti kuwa upo wosia uliosainiwa na Epstein, unaoonesha kuwa watoto wa Mona, kila mmoja atapa Dola 5 milioni (Sh13 bilioni) za urithi kutoka kwa mhalifu huyo wa ngono.
Peter Mandelson, aliyekuwa Balozi wa UK nchini Marekani, alifukuzwa kazi baada ya toleo la mapema la Mafaili ya Epstein, kuonesha ukaribu wake na mhalifu huyo ngono kwa mabinti wadogo mwaka 2015.
Baada ya toleo jipya la nyaraka Januari 30, 2026, Mandelson alilazimika kujiuzulu ujumbe wa chemba ya juu ya Bunge la UK, House of Lords.
Nyaraka zimeonesha uhusiano wa karibu baina ya Mandelson na Epstein. Vilevile, Mandelson ambaye ni shoga, na mume wake, Reinaldo Avila da Silva, walikuwa wakipokea misaada ya kifedha kutoka kwa Epstein.
Kathy Ruemmler ni mwanasheria daraja la juu Marekani. Februari 12, 2026, alitangaza kwa umma kuwa Juni 2026, ataachana na Benki ya kimataifa ya Goldman Sachs, ambayo yeye ndiye mwanasheria mkuu.
Uamuzi huo umefuatia mawasiliano yake ya barua pepe na Epstein kuwekwa wazi na DOJ. Kathy alilimbia Gazeti la Financial Times kuwa anaondoka kazini baada ya kuandamwa na vyombo vya habari.
Awali, Kathy alisema asingeacha kazi hiyo kisa kutajwa kwenye Mafaili ya Epstein.
Hata hivyo, presha kubwa kutoka kwenye vyombo vya habari imemlazimisha. Nyaraka za Mafaili ya Epstein zimeonesha jinsi Kathy alivyokuwa anapokea zawadi kutoka kwa bilionea huyo mhalifu wa ngono kwa watoto wadogo.
Vyombo vya habari vimekuwa vikikuza maneno “Uncle Epstein”, baada ya mafaili kuonesha Kathy alivyokuwa akimwita Epstein.
Watu wa Canada nao hawajaachwa salama. Mwanazuoni mwenye heshima kubwa nchini humo na Marekani, Lee Smolin, amesimamishwa kazi Chuo Kikuu cha Waterloo, kilichopo Ontario.
Taarifa ya Waterloo ilieleza kuwa, uamuzi huo ulikuwa makubaliano ya pamoja, baina ya uongozi wa chuo na Profesa Smolin.
Jina la Smolin limejitokeza mara 182 katika nyaraka za kwenye Mafaili ya Epstein, zilizowekwa wazi hadi sasa.
Inafahamika kuwa kutajwa pekee kwenye Mafaili ya Epstein, hakuna maana kuwa tayari ni mhalifu.
Hata hivyo, mawasiliano yoyote yaliyofanyika dhidi ya Epstein, baada ya kukutwa na hatia ya uhalifu wa kingono kwa watoto wadogo mwaka 2008, yamekuwa yakitengeneza maswali tata.
Profesa Smolin aliwasiliana na Epstein hata baada ya mhalifu huyo kuhukumiwa na kufungwa jela miezi 18.
Shauku ya wengi ni orodha zaidi kuendelea. Maana kuna zaidi ya kurasa milioni tatu hazijawekwa wazi.
Majina mengi ya watu yamezibwa, pamoja na anuani. Uhariri ni mkubwa katika nyaraka zilizoachiwa. Kitendo cha kupiga danadana, kimekuwa kikisababisha wasiwasi mkubwa kwa Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye ametajwa mara nyingi kwenye mafaili na alikuwa swahiba wa Epstein. Je, nyaraka zaidi zitaachiwa? Majina na anuani vitafichuliwa? Ni kweli Trump analinda makosa yake? Muda utanena!