Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imesema kwa sasa kila maiti inayotoka nje ya nchi kuja nchini, inakaguliwa kubaini iwapo haijatumika kama chombo cha kusafirisha dawa hizo.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema hatua hiyo inatokana na kubainika mbinu ya matumizi ya maiti kusafirisha dawa za kulevya, hivyo katika viwanja vya ndege imefungwa mdaki  (scanner) maalumu kwa ajili ya ukaguzi.  

Lyimo ametoa kauli hiyo hivi karibuni, alipozungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu yaliyofanyika makao makuu ya mamlaka hiyo, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa za kiuchunguzi, baadhi ya maiti zilipasuliwa tumboni kuondolewa utumbo na nyingine kufunguliwa fuvu la kichwa kuondolewa ubongo na kujazwa dawa za kulevya.

Lyimo  amesema baada ya udhibiti wa usafirishaji wa dawa za kulevya kwa njia ya kumeza, wakaibua mbinu ya kusafirisha kwa kutumia maiti.

“Mtu akishafariki, wanapasua tumbo wanajaza dawa za kulevya, au wanafunua fuvu wanaweka dawa za kulevya na wanafunika na gundi huwezi kugundua,” amesema Lyimo.

Baada ya kugundua hilo, amesema wameweka mdaki katika viwanja vya ndege na kuanzia sasa, kila maiti inayosafirisha inaskaniwa ili kuona iwapo tumboni au kichwani kuna chochote.

Kutokana na ukaguzi huo, Lyimo amesema mwaka 2024 walikamata maiti iliyotoka Afrika Kusini kuingia nchini, ikiwa imejazwa dawa za kulevya ndani yake.

“Walifunua kichwa wakatoa ubongo wote wakajaza dawa za kulevya, kwenye tumbo walitoa utumbo wote wakajaza dawa kwa hiyo unakuta maiti imekuja watu wanaenda kuzika kumbe ina dawa za kulevya,” amesema.

Kutaifisha, kutekeleza 

Uamuzi wa kutaifisha mali za wafanyabiashara wa dawa za kulevya, amesema ulianza baada ya kubaini wengi wao wakikamatwa na kufungwa, wanapotoka hutumia mali hizo kurudi kwenye biashara hiyo haramu.

Hatua hiyo, amesema ikailazimu Serikali ibadili sheria na kuruhusu utaifishaji wa mali za mtuhumiwa alizozipata ndani ya kipindi cha miaka 10 nyuma kuanzia siku aliyokamatwa.

Ameeleza kwa kipindi cha miaka 10, DCEA imetaifisha mali za Sh3.3 bilioni zilizotokana na watuhumiwa wa dawa za kulevya zikihusisha vitu mbalimbali.

Akizungumzia utaratibu wa utaifishaji, Lyimo amesema ukishafungua jalada la kesi ya msingi ambayo ni dawa za kulevya, pia linafunguliwa lingine la utaifishaji mali.

“Mali zote ambazo mtuhumiwa amezipata ndani ya miaka 10, zinahusishwa kuwa ni zao la dawa za kulevya. Kesi ya msingi ya dawa za kulevya ikishaamriwa, inafuata kesi ya msingi ya utaifishaji mali,” amesema.

Wakati mwingine, amesema jalada la utaifishaji mali hufunguliwa kama imethibitika kuwa mtu huyo ni mfanyabiashara wa dawa za kulevya lakini amekimbia au hajakamatwa, hivyo mali zake zitataifishwa na atakapokamatwa kesi ya msingi itaendelea.

Baada ya mali hizo za watuhumiwa kutaifishwa, amesema zinawasilishwa kwa Msajili wa Hazina ambaye ndiye mmiliki wa mali za Serikali na huko ndiko itakapopangwa zitumike vipi.

Maiti zinavyotumika kusafirisha dawa za kulevya

“Yeye sasa anaangalia kama anazipiga mnada fedha zinaingia serikalini, au kama kuna mali zinazoweza kutumika kwa matumizi ya Serikali basi yeye ndiye anayetoa kibali. Sisi hatuna mamlaka ya kuzitumia hadi tuombe kibali hazina, kwa hiyo tunakabidhi kwake,” amesema.

Uteketezaji dawa za kulevya

Pia, amesema baada ya kukamata dawa na kesi kuhukumiwa, Mahakama hutoa kibali cha kuteketezwa. Lakini kabla ya hatua hiyo, zitapimwa kujua iwapo ni kiwango kile kile kama zilivyoelezwa kwenye jadala la kesi.

Zikishapimwa kwa ukubwa, amesema pia hupimwa na Mkemia Mkuu wa Serikali pakiti moja baada ya nyingine ili kuhakikisha kuwa ni dawa za kulevya na hakuna iliyobadilishwa.

“Ikishapimwa yote na kuthibitika, sasa hapo ndipo zinateketezwa. Lakini kuna dawa za kulevya zinazoteketezwa kabla ya kesi kuhukumiwa. Mfano mirungi na nyingine ambazo huharibika haraka,” amesema.

Vivyo hivyo, amesema inafanyika katika uteketezaji mashamba ya bangi kwa kuwa, mara nyingi mzigo huwa mkubwa na inashindikana kuubeba, hivyo jadala linafunguliwa na hakimu anakwenda shambani kushuhudia uteketezaji.

Alipoulizwa iwapo zote zinateketezwa na hakuna zinazobadilishiwa matumizi, amesema kila dawa ya kulevya inayoingizwa kwa matumizi hayo, zinateketezwa na hazibadilishiwi matumizi hata kama zinaweza kuwa na msaada kwenye eneo jingine.

“Serikali ina utaratibu wake wa kuingiza dawa za tiba, kama hizi zimechepushwa na kuingizwa ili zitumike kama dawa za kulevya, tunateketeza zote kwa kuwa huwa zinaingia kinyume cha sheria,” amesema.

Kuchelewa kesi za dawa za kulevya

Alipoulizwa kuhusu kuchelewa kwa kesi hizo, amesema mara nyingi zina mchakato unaochukua muda mrefu hadi mtu atiwe hatiani, kwa kuwa adhabu zake ni kubwa.

“Unapokamata mtu ana mirungi lazima uthibitishe kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwamba ile ni mirungi, lazima mali yake itaifishwe, hapo utahusisha Wizara ya Ardhi kuthibitisha kuwa ardhi ni yake, chombo cha usafirishaji lazima uthibitishe kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),” amesema.

Amesema kila taasisi itatumiwa barua ifanye uchunguzi na kutoa mrejesho wa kuthibitisha kama mali husika inahusiana na mtuhumiwa kwa ajili ya hatua za kisheria.

“Hadi kuthibitisha hiyo, inachukua muda mrefu ndio maana unasikia upelelezi haujakamilika. Huwa kunakuwa na mchakato mrefu kabla ya kukamilisha nyaraka hizo,” amesema.

Kuhusu skanka

Lyimo amesema kwa sasa kuna msukumo wa Dunia kuishawishi Afrika ilime bangi kwa madai itakua kiuchumi na kwamba kuna ahadi ya kununua kwa gharama kubwa.

Ushawishi huo, amesema umesababisha baadhi ya mataifa kuridhia kulima zao hilo ikiwamo Malawi, Eswatini na Afrika Kusini.

Lakini amesema kila ushawishi uliofanyika ulikuwa mtego akitolea mfano Malawi, ambako baadhi ya Watanzania walikwenda kulima bangi baada ya kunyimwa vibali nchini.

“Walikuja Watanzania kuomba kibali walime bangi wakakokotoa kwamba Serikali itapata kodi kubwa, tukakataa baada ya kufanya tathmini na kubaini faida ni ndogo ukilinganisha na hasara,” amesema.

Amesimulia kuhusu Mtanzania aliyekwenda kulima nchini Malawi. Aliuza nyumba zake na baadhi ya mali apate mtaji wa Sh300 milioni kwa ajili ya kilimo cha bangi nchini humo.

Baada ya kulima, amesema Malawi imeuza bangi zisizozidi asilimia 40 na nyingine zote zimebaki stoo, huku yule Mtanzania aliyekwenda kulima nchini humo zake hazikuuzwa kabisa.

“Kwa sasa amechanganyikiwa, alichukua mkopo kwa sasa amepooza, anaomba msaada na tumemsaidia kwa kumnunulia mashine ya kutembelea,” amesema.

Kwa kuwa wateja walioahidi kununua hawakutokea, amesema wakawaletea teknolojia ya kusindika na kemikali na inatokea bangi kali ambayo ndiyo inakuwa skanka.

“Bangi ya kawaida inakuwa na THC 2 hadi 12 au 13 yaani kiwango cha sumu, lakini skanka inakuwa na THC 40 hadi 60 na bidhaa zinazotengenezwa na skanka zinakuwa na THC hadi 90, kuna pipi tulikamata Mbeya, tulivyopima moja ilikuwa na THC 90. Fikiria ile sumu ipo kwa kiwango hichom mtu akitumia anakuwa katika hali gani,” amesema.

Amesema Tanzania haitengenezi skanka badala yake zinatoka katika mataifa yaliyolima zao hilo ambayo ni Malawi na Eswatini na DCEA inadhibiti bidhaa hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *