Baada ya kushindwa kupachika bao katika mechi 21 mfululizo za mashindano tofauti, Fiston Mayele jana, Februari 24, 2026 amemaliza ukame wa mabao baada ya kuifungia Pyramids FC katika ushindi wa mabao 3-1 ambao imepata ugenini dhidi ya Ghazl El Mahallah katika mchezo wa Ligi Kuu ya Misri.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, amepachika bao hilo katika dakika za majeruhi za mchezo huo, akimalizia pasi ya Mahmoud Zalaka na kuihakikishia ushindi huo, Pyramids FC ambao umeisogeza hadi katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.

Bao hilo moja limemfanya Mayele aandike rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya Pyramids FC kufunga mabao 50 katika mashindano tofauti.

Katika mchezo huo, mabao mengine ya Pyramids FC yamepachikwa na Nasser Mayer na Mostafa Fathi huku bao pekee la kufutia machozi la Ghazl El Mahallah likipachikwa na Sunday Williams.

Ikumbukwe kabla ya mechi ya jana, mara ya mwisho kwa Mayele kufunga bao ilikuwa ni Oktoba 21 mwaka jana katika mchezo dhidi ya Pharcowa Ligi Kuu ya Misri.

Katika michezo hiyo 21 mfululizo ambayo Mayele hakufunga bao, mechi 15 zilikuwa ni za mashindano ya Klabu na michezo iliyobaki sita ni ya timu ya taifa.

Mshambuliaji wa Pyramids FC na timu ya taifa ya DR Congo, Fiston Mayele. Picha na Pyramids FC

Msimu uliopita ulionekana kuwa mzuri kwa Mayele baada ya kuibuka kinara wa kufumania nyavu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akipachika mabao sita.

Mabao hayo sita yalitoa mchango mkubwa katika kuiwezesha Pyramids FC kutwaa taji la mashindano hayo ikifanya hivyo kwa mara ya kwanza.

Mayele siku chache baadaye aliiongoza Pyramids FC kutwaa ubingwa wa mashindano ya FIFA ya klabu za Asia, Afrika na Oceania baada ya kuifungia mabao matatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *