Iringa. Furaha na shangwe zimetawala katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, baada ya watu 13 wenye ulemavu kukabidhiwa viungo bandia vya miguu vilivyogharimiwa na Mbunge wa Kilolo, Ritta Kabati kupitia Taasisi ya Ritta Kabati Trust Fund.

Wanufaika hao wamesema kwa muda mrefu walikwamishwa na gharama kubwa za viungo saidizi, hali iliyowafanya waendelee kuishi kwa utegemezi na changamoto za kimwili na kiuchumi.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Februari 25, 2026, wamesema  msaada huo ni chanzo cha matumaini mapya baada ya kukabiliwa na changamoto za ulemavu kwa muda mrefu.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Ibrahimu Swedi (29) mkazi wa Don Bosco, Manispaa ya Iringa, amesema msaada huo utabadili mwelekeo wa maisha yao na kuwapa nafasi ya kusimama tena kwa kujiamini.

“Kwa muda mrefu tulikuwa tegemezi, lakini leo tunaanza ukurasa mpya. Mguu bandia huu si kifaa tu, bali ni maisha mapya,” amesema Swedi.

Naye Alfred Mtandi (39), mkazi wa Image wilayani Kilolo, amesema kutumia magongo kulimkwamisha katika shughuli zake nyingi za kila siku, hususan biashara ndogo aliyokuwa akiifanya kwa lengo la kujipatia kipato.

“Nilishindwa kusimama kwa muda mrefu, hali iliyokuwa inanisababishia kupoteza wateja. Sasa nina uhakika wa kurejea kazini na kuendesha maisha yangu bila aibu,” amesema Mtandi.

Kwa upande wake, Jacob Mwenda (59) kutoka Mgama, Wilaya ya Iringa, amesema kutokana na umri wake, kutumia magongo kulimsababishia maumivu makali ya mgongo na uchovu wa mara kwa mara.

“Sasa naweza kutembea kwenda ibadani na kutimiza majukumu ya kifamilia bila mateso niliyokuwa nayapitia,” amesema Mwenda.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kabati amesema taasisi yake imekuwa mstari wa mbele kusaidia watu wenye mahitaji maalumu tangu mwaka 2020, ambapo zaidi ya watu 300 wamenufaika na misaada mbalimbali.

Amesema ulemavu haupaswi kuwa kikwazo cha kutimiza ndoto za mtu na ameahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuwafikia wahitaji wengi zaidi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Estomin Kyando amemshukuru mbunge huyo pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa ushirikiano wao, akieleza kuwa juhudi hizo zinaendana na sera za kitaifa za kuwajali watu wenye mahitaji maalumu.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Alfred Mwakalebela, ametoa wito kwa wadau wengine wa sekta ya afya kujitokeza kusaidia ili kupanua wigo wa huduma kwa makundi maalumu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *