
Dar es Salaam. Wakati Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ikiendelea kuvitupia lawama vyama na viongozi wake kwa kuibua migogoro kutokana na kutokuzingatia katiba na maadili yao huku ikichukua hatua za kinidhamu mara kadhaa, hali ya mivutano ndani ya vyama hivyo imeendelea kushika kasi.
Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa vyama wamekuwa wakimrushia lawama Msajili wakimtuhumu kuwa sehemu ya chanzo cha migogoro hiyo. Wakati mvutano huo ukiendelea, wataalamu na wachambuzi wa siasa wamefungua mjadala mpana wakizitazama hoja za pande zote mbili.
Tangu enzi za TANU hadi vyama vilivyofuata kama Chama cha Mapinduzi (CCM), Civic United Front (CUF), NCCR Mageuzi, Tanzania Labour Party (TLP), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT – Wazalendo na vingine vingi, historia inaonesha karibu kila chama kimewahi kupitia misukosuko ya aina yake, iwe ni ya ndani au inayohusisha mamlaka za dola.
Hali hiyo imejenga hoja kuwa migogoro si jambo jipya wala si la chama kimoja pekee, bali ni sehemu ya mchakato wa kisiasa nchini.
Wataalamu wa siasa na utawala bora wanasema migogoro ya vyama ina mizizi ya kihistoria na kwa kiasi kikubwa hutokana na mgongano wa kimaslahi na kimtazamo ndani ya mfumo wa demokrasia. Wanaeleza kuwa demokrasia inaruhusu ushindani wa mawazo, lakini ushindani huo usiposimamiwa kwa misingi ya kitaalamu na kisheria, huweza kugeuka chanzo cha migawanyiko.
Kwa mujibu wa wachambuzi hao, sababu kuu za migogoro ni pamoja na ubinafsi wa baadhi ya viongozi, kung’ang’ania madaraka, kutokuelewana katika tafsiri ya katiba za vyama, tofauti za maono, pamoja na migongano ya maslahi ya makundi mbalimbali ndani ya chama.
Aidha, suala la kuingiliwa kwa vyama na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa limekuwa likitajwa kama kichocheo kingine cha migogoro, hasa pale vyama vinapohisi hatua zinazochukuliwa si za haki au hazina usawa.
Hoja za viongozi wa vyama
John Heche, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, ameielekezea lawama Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, akiituhumu kwa kile anachodai ni kuhujumu vyama vya upinzani.
Anasema ofisi hiyo imepanua mamlaka yake zaidi ya jukumu la msingi la kusajili vyama na kujigeuza chombo kinachotoa maamuzi yanayofanana na ya kimahakama, ikiwa ni pamoja na kufungia shughuli za vyama, kuzuia mikutano na kutoa maonyo kwa barua na matamko.
Kwa mtazamo wake, ili kuondoa mvutano uliopo, kunahitajika marekebisho ya kimuundo yatakayobaki na taasisi ya usajili pekee, huku migogoro mingine ikipelekwa katika vyombo halali vya utoaji haki kama mahakama.
Heche anadai pia kuwa kuna ushahidi wa madai kwamba ofisi hiyo imekuwa ikitumia mbinu za kuchochea migogoro ndani ya vyama, kisha kuchukua hatua za kinidhamu kama sehemu ya mkakati wa kuvinyong’onyeza.
Heche anaongeza kuwa kutokuelewana ndani ya vyama ni jambo la kawaida katika mchakato wa kidemokrasia, ambapo maoni ya wengi hufuata taratibu huku wachache wakipewa nafasi ya kusikilizwa.
Hata hivyo, anaona tatizo kubwa likiwa ni namna Msajili anavyoshughulikia vyama vya upinzani, akidai kuwa kuna upendeleo katika utekelezaji wa hatua.
Mtazamo wa Ofisi ya Msajili
Hata hivyo, wakati baadhi ya viongozi wa vyama wakiishutumu Ofisi ya Msajili kwa kile wanachodai ni kuchochea migogoro kupitia mamlaka yake ya usimamizi, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza amezungumza na Mwananchi na anasema chanzo kikuu cha migogoro ni wanachama kushindwa kuheshimu katiba na kanuni za vyama vyao pamoja na Sheria ya Vyama vya Siasa.
Nyahoza anabainisha kuwa ingawa mivutano haiwezi kuisha kabisa kwa kuwa husababishwa na sababu mbalimbali, msingi wa utatuzi wake ni kufuata katiba, kanuni na sheria walizojiwekea.
Kwa mujibu wake, Ofisi ya Msajili imekuwa ikitoa miongozo kwa kusisitiza uzingatiaji wa misingi hiyo, akifananisha uendeshaji wa vyama na taasisi nyingine kama Saccos ambazo huongozwa kwa mujibu wa katiba zao.
Kwa upande wake, Ado Shaibu, Katibu Mkuu wa Chama cha ACT – Wazalendo, anasema migogoro ya vyama haiwezi kutoweka kabisa kwa kuwa ni sehemu ya historia ya siasa, si nchini tu bali hata katika vyama vya kimataifa kama African National Congress (ANC) na hata katika harakati za kisiasa za Zanzibar kama UMMA Party.
Anataja sababu kuu mbili za migogoro kuwa ni mgongano wa maslahi ndani ya vyama na kile anachokiita mkono wa dola.
Kwa mujibu wake, suluhisho la kudumu ni vyama kuwa na itikadi imara inayotekelezwa kwa vitendo, wanachama kuishi misingi hiyo, na kuwekeza katika utatuzi wa migogoro kwa njia za kisheria.
Pia anasisitiza umuhimu wa kuvumiliana katika tofauti za maoni na mitazamo, akiamini kuwa hatua hizo zitapunguza athari za migogoro inapojitokeza.
Naye John Mrema, Msemaji wa Chama cha Umma (Chaumma), anavitazama vyama vya siasa kama taasisi zinazoundwa na watu wenye hulka, mitazamo na malengo tofauti.
Anasema baadhi ya wanachama hujiunga kwa lengo la kupata nafasi za uongozi na wanaposhindwa huzua migogoro au kuondoka. Wengine huingia wakiwa na dhamira ya kutatua changamoto wanazoziona katika jamii.
Anabainisha kuwa katiba za vyama ndizo msingi wa umoja na migogoro huibuka pale katiba hizo zinapokiukwa au kupuuzwa na viongozi wanaotumia mamlaka badala ya ushawishi.
Aidha, ushindani wa kisiasa kati ya vyama nao huchochea mikakati ya kudhoofishana, jambo linaloweza kuzaa migogoro ya ndani na nje ya vyama.
Kwa ujumla, mjadala unaibuka ni iwapo chanzo cha migogoro ni udhaifu wa mifumo ya ndani ya vyama au namna mamlaka za usimamizi zinavyotekeleza majukumu yake.
Wakati pande zote zikiendelea kutupiana lawama, wataalamu wanasisitiza haja ya kuimarisha misingi ya kikatiba, uwazi na utawala wa sheria ili demokrasia ya vyama iweze kustawi bila migawanyiko isiyokuwa ya lazima.
Akifafanua kwa upana kuhusu mizizi ya migogoro ndani ya vyama vya siasa, mmoja wa wachambuzi anasema ukiyachunguza makundi yanayounda vyama utaona wazi kuwa vyanzo vya migogoro ni vingi na hutofautiana kulingana na wakati na mazingira husika.
Anaeleza kuwa katika sayansi ya siasa, njia bora ya kukilinda chama ni kuhakikisha viongozi wake hawajiegemezi kwa kundi moja na kulisahau jingine.
Kwa mtazamo wake, viongozi wanapaswa kusimama katikati ya makundi yote, wakitambua mahitaji na matarajio ya wanachama wao na kuyatumia kuongoza dhamira ya chama.
Anasisitiza kuwa migogoro haiwezi kutoweka kabisa ndani ya vyama vya siasa, bali inaweza kupunguzwa kwa kuanzisha mifumo thabiti ya kuibaini na kuishughulikia mapema kabla haijakua na kukidhoofisha chama.
Aidha, anaeleza kuwa vyama ni taasisi zinazobadilika kulingana na wakati, hivyo vinapaswa kuwa tayari kupokea mawazo na maoni mapya, hata kama hayawapendezi viongozi waliopo.
Kila siku vyama hupokea wanachama wapya wenye mitazamo na maslahi tofauti, jambo linalohitaji uongozi wenye uvumilivu na uwezo wa kusikiliza. Kabla ya kufanya maamuzi makubwa ya kisera au kimwelekeo, anashauri viongozi kuwashirikisha wanachama wao na kutumia ushawishi badala ya mamlaka ya amri.
Kwa upande wake, Hassan Doyo, Katibu Mkuu wa National League for Democracy (NLD), anasema baadhi ya viongozi wanapokuwa madarakani hukosa utashi wa kisiasa wa kuimarisha vyama vyao zaidi ya kulinda nafasi zao binafsi.
“Kutovumiliana katika mitazamo ya kiuongozi, uroho wa madaraka na maslahi binafsi ni miongoni mwa sababu zinazoendeleza migogoro ndani ya vyama,” anasema Doyo.
Anasisitiza umuhimu wa mabadiliko ya kimtazamo kwa viongozi, akiwataka kuacha tamaa ya uongozi wa kudumu na ubinafsi, na badala yake kukubali mawazo mapya pamoja na kujenga utamaduni wa uvumilivu katika uongozi.
Mitazamo ya wachambuzi na wasomi
Denis Konga, mhadhiri wa Abeid Karume Institute of Diplomacy, anasema vyama vingi huanzishwa kama vuguvugu la kutetea maslahi ya watu fulani yanayohusishwa na mahitaji ya wengi.
Hata hivyo, anataja kuwa udhaifu wa misingi ya uanzishwaji wake unaweza kuathiri uendeshaji wake baadaye.
Anasema iwapo msingi wa chama ni dhaifu, hata demokrasia ya ndani huwa dhaifu. Waanzilishi wanapojiona wamiliki wa chama, huweza kuwapuuza wanachama wengine kwa hoja ya kuwa wao ndio waliokiasisi.
Aidha, anataja uwezekano wa baadhi ya viongozi kuwa na maslahi yanayokinzana na dhamira ya chama, hali inayochochea kutokuaminiana na ushindani wa ndani. Konga pia anagusia kupotea kwa itikadi kama chanzo kingine cha migogoro. Anasema wanachama wengi hujiunga bila kuelewa misingi ya chama chao. Vilevile, anaonya dhidi ya hali ya kukipa chama sura ya mtu mmoja maarufu badala ya taasisi.
Anatoa mifano ya Civic United Front (CUF) kuhusishwa na Ibrahim Lipumba, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusishwa na Tundu Lissu au Freeman Mbowe, na hata Chama Cha Mapinduzi kumtegemea zaidi mwenyekiti wake.
“Hali hiyo ndiyo huzaa migogoro pale mtu anapokuwa mkubwa kuliko taasisi,” ansema.
Aidha, anataja kinga ya kisheria ya Ofisi ya Msajili dhidi ya kushtakiwa kama hoja inayochochea mjadala, akitolea mfano mchakato wa kuondoka kwa Lipumba katika uongozi wa CUF uliogubikwa na mabishano kufuatia barua ya Msajili.
Kwa upande wake, Paul Loisulie, Mhadhiri wa University of Dodoma (UDOM) anasema uchanga wa uongozi na wanachama, pamoja na ukosefu wa uzoefu wa kuendesha taasisi za kisiasa, ni miongoni mwa sababu za migogoro, hasa kwa vyama vinavyoanza.
Anaongeza kuwa ubinafsi wa viongozi na ukosefu wa maono ya pamoja huongeza migawanyiko.
Dk Loisulie pia anagusia kutokuwepo kwa usawa wa kisiasa katika mazingira ya ushindani, akisema vyama vya upinzani havipati fursa sawa na chama tawala.
Hata hivyo, anaamini kuwa kadri mwamko wa jamii unavyoongezeka na mabadiliko ya kisheria na kikatiba yanavyofanyika, mazingira ya kisiasa yataimarika na kupunguza migogoro.
Naye mchambuzi wa siasa, Faraji Mangula anaonya kuwa kung’ang’ania madaraka kunadhoofisha demokrasia barani Afrika.
Anawahimiza wanasiasa waliokaa madarakani kwa muda mrefu kuwa tayari kupisha wengine kwa hiari ili kuepusha migogoro na machafuko yanayoweza kuvuruga imani ya wananchi kwa vyama vya siasa, hali inayoweza pia kuathiri chaguzi zijazo, ikiwamo ile ya mwaka 2030.